December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walipa kodi Tabora waunga mkono juhudi za Rais Samia

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Tabora imeeleza kupata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 3 ya utawala wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na mwitikio mzuri wa wananchi kulipa kodi.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mamlaka hiyo Mkoani hapa Fredrick Kanyilili alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake juzi ambapo alibainisha kuwa kasi ya ulipaji kodi imeendelea kuongeza kila mwaka.

Ameeleza kuwa TRA Mkoa imefanikiwa kusajili walipa kodi wapya wapatao 12,512 katika kipindi hicho ambapo walipa kodi 4,813 walisajiliwa kwa mwaka 2020/2021, walipa kodi 3,726 mwaka 2021/2022 na 3,973 kwa mwaka 2022/2023.

Meneja ameongeza kuwa Mamlaka hiyo ilipangiwa kukusanya sh bil 76.9 kwa miaka 3 ambapo kwa mwaka 2020/2021 ilipaswa kukusanywa sh bil 24.82 lakini wakakusanya bil 24.7 sawa na asilimia 99.7, mwaka 2021/2022 sh bil 26.45 lakini wakakusanya sh bil 22.2 sawa na asilimia 83.8.

Mwaka 2022/2023 walipanga kukusanya sh bil 25.7 lakini wakapata sh bil 24.6 sawa na asilimia 95.9 na kuanzia Julai 2023 hadi Februari 2024 walipanga kukusanya sh bil 12.3 kwa wateja wa kati pekee lakini wakakusanya bil 12.9 sawa na asilimia 105.

Kanyilili amedokeza kuwa miaka 3 ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa na mwitikio mzuri sana wa ulipaji kodi na kiwango cha makusanyo kimeendelea kuongezeka kila mwaka.

‘Tunawashukuru sana walipa kodi wa Mkoa wa Tabora kwa mwitikio wao mzuri katika ulipaji kodi, katika hili wameunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za kuwaletea maendeleo Watanzania’, ameeleza.

Aidha amesema kuwa katika kipindi cha miaka 3 tangu Rais Samia aingie madarakani, Mamlaka hiyo imefanikiwa kuwa na Ofisi katika Wilaya zote 7 za Mkoa huo huku Wilaya ya Uyui ikihudumiwa na Ofisi ya Tabora Manispaa.

Amefafanua kuwa mbali na kuwa na Ofisi katika Wilaya hizo jengo la Ofisi za TRA Mkoa nalo linafanyiwa ukarabati mkubwa ili kuwa na mwonekano bora zaidi, jengo hili litakuwa kichocheo kikubwa cha kasi ya utendaji wa Mamlaka hiyo.

Akiongea kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake wa Mkoa huo Hussein Kafwenda amesema kuwa Rais Samia anafanya kazi nzuri na kodi wanazolipa zinatumika vizuri, hivyo wataendelea kumuunga mkono kwa kulipa kodi stahiki.

Amebainisha kuwa wafanyabiashara hawana ugomvi na TRA ila akashauri Maafisa wake kujenga mahusiano mazuri na walipa kodi na sio kutumia lugha za maudhi au kubambikiza kodi kinyume na utaratibu.