Na Zuhura Zukheir, TimesMajira Online, Iringa
VIONGOZI waliochaguliwa katika mchakato wa kura za maoni mkoani Iringa kupitia Jukwaa la Wanawake wa CCM Tanzania UWT wametakiwa kuhakikisha wanatekeleza ahadi zao walizozitoa wakati wakiomba kura na kuacha kutokomea na kurudi baada ya miaka mitano kwa kutegemea kununua uongozi.
Rai hiyo imetolewa na msimazi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi alipokuwa anatangaza matokeo ya uchaguzi wa viti maalum na makundi mbalimbali mkoani Iringa ambapo aliwataka wanachama walioanguka katika chaguzi hizo kuwa watulivu kwa kuwa wanaweza kupata wakati mwingine.
Hapi amewataka wajumbe wa UWT Mkoa wa Iringa kuendeleza umoja wao hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu ili kwenda kusaidia kutafuta ushindi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 28 mwaka huu.
Aidha amewataka wajumbe na wanachama wa chama cha mapinduzi ccm wilaya ya Iringa kuhakikisha wanafanya kazi ya chama kwa nguvu zote na hatimae kulirudisha jimbo mikononi mwa chama cha Mapinduzi CCM.
Hapi aliwapongeza wagombea wote waliojitokeza kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchukua fomu na kugombea,ambapo amesema wote walioshindwa na walioshinda wana haki sawa na wanatakiwa kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya kukijenga chama cha mapinduzi.
Baada ya kuyasema hayo na kuwapongeza wagombea waliojitokeza alitangaza matokeo ya walioongoza katika kura za maoni ambapo katika nafasi ya ubunge wa viti maalum wanawake aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum Iringa Rose Tweve alishika nafasi ya kwanza kwa kupata kura 215, akifuatiwa na aliyekuwa mbunge wa viti maalum Ritha Kabati akipata kura 198 huku Nance Nyalusi akishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 136.
Mwanahabari Jema Mdegela ambaye ni mdogo wa muigizaji maarufu Tausi Mdegela ameshinda ubunge kupitia kundi la walemavu kwa kupata kura 215 nafasi ya pili ikishikwa na Jesca Mwaliyoyo aliyepata kura 59 na nafasi ya tatu akishika Teodora Tagilavanu.
Kwa upande wa kundi la wasomi aliyeongoza ni Tafuteni Chusi aliyepata kura 148 nafasi ya pili Cythia Zocca kapata kura 42 huku nafasi ya tatu ikishikwa na Godliver Mvanda akipata kura 65.
Akitangaza matokeo ya washindi wa kundi la wafanyakazi Mkuu wa Mkoa wa Iringa alimtangaza Catherine Charwe kuongoza kwa kupata kura 74 nafasi ya pili akitangazwa Hanna Kibopile akipata kura 70 na Saida Mgeniakipata kura 52.
Aidha alitangaza matokeo ya kundi la wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali NGO’s ambapo muigizaji maarufu hapa nchini Halima Mpinge (Davina) akiongoza kwa kupata kura 164,nafasi ya pili ikishikwa na Faith Dewasi aliyepata kura 48 na nafasi ya tatu akipata Stellah Mdahila aliyepata kura 35.
Wagombea wote walikubali matokeo na kusaini fomu ya wagombea huku walioongoza katika mchakato huo wakisema kuwa uchaguzi haukuwa mwepesi kwa kuwa ulikuwa haujafahamika nani anaweza kupata nafasi kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao wagombea wote katika kunadi sera zao jukwaani.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti