January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliohitimu JKT watakiwa kutovuruga amani

Na Fresha Kinasa, TimesMajira Online, Mara

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Nchini Meja Generali Charles Mang’era Mbuge, ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kugharamia mafunzo kwa Vijana Nchini ambayo amesema yamekuwa chachu ya kuwajengea uzalendo, uadilifu na uwajibikaji kupitia uzalishaji mali kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Meja Generali Mbuge ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya mujibu wa sheria 2020 Operesheni Uchumi wa kati katika kikosi cha 822 KJ Rwamkoma Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara, ambapo pamoja na mambo mengine, aliwataka wahitimu hao kuyatumia maarifa waliyoyapata kwa manufaa ikiwemo kuwa wazalendo, waadilifu na kulitumikia Taifa kwa uadilifu mkubwa.

“Naishukuru serikali kwa kuendelea kugharamia mafunzo haya kwa vijana, hakika vijana wanaendelea kupata maarifa na ujuzi ambao unafaida katika maisha yao wanapohitimu, niwaombe vijana wote kazingatieni mliyofundishwa mkaoneshe tabia njema na mienendo inayofaa ikiwemo utii, uadilifu na kutotumiwa hata kidogo kuvuruga amani hususan kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, kaweni mabalozi wema wa Jeshi la Kujenga Taifa katika vyuo mtavyokwenda kusoma masomo yenu na hata baada ya masomo pia, ” amesema.

Pia amewataka wahitimu hao kuondokana na mtazamao hasi kwamba, JKT ni sehemu ya ajira, bali watambue ni sehemu ya kuwapika vijana wapate ujuzi na maarifa ambayo yatawezesha kuwajenga katika kujitegemea juu ya masula mbalimbali yenye manufaa yao katika kuwainua kiuchumi na kuwaweka tayari wakati wote kuwa na uzalendo kwa Taifa na rasilimali zilizipo.

Wahitimu wa mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria Operesheni uchumi wa kati 2020 katika kikosi cha 822KJ Rwamkoma Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara wakipita kutoa heshima kwa Mkuu wa Jeshi hilo Nchini Meja Generali Charles Mang’era Mbuge (hayupo pichani) alipofika kufunga mafunzo hayo. ( Picha na Fresha Kinasa)

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo, AKH 7695 SG Mariam Haruna amesema, walianza mafunzo hayo wakiwa 938, na waliofanikiwa kuhitimu ni 933, huku wengine watano wakishindwa kuhitimu mafunzo hayo kwa sababu ya utoro.

Amesema, wamejifunza mambo mbalimbali ikiwemo ukakamavu, uzalendo, uadilifu, ushirikiano, utii, uaminifu, pamoja na shughuli za Ujasiliamali, kutunza mazingira na uzalishaji mali, ambapo kwa muda mfupi alisema wameweza kuotesha miche 85,000 kwa muda mfupi, huku akisema kwamba watazingatia yote waliyofundishwa mafunzoni.

Aidha ameiomba serikali kuongeza muda wa mafunzo hayo uweze kuongezwa kutoka miezi miwili hadi miezi sita ili kujifunza mambo mengi kwa ufanisi, ambapo pia aliishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha mafunzo hayo kwa vijana kwa mujibu wa sheria na akaahidi kwamba wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kutunza na kulinda amani nchi na kukuza uchumi wa Taifa.

Kaimu Kamanda wa kikosi cha 822 KJ Rwamkoma Luteni kanali Gaudencia Mapunda alisema mafunzo hayo yamechukua miezi miwili, ambapo alisema matarajio ni kuona vijana hao wanakwenda kuyatumia kwa faida mafunzo hayo kama ambavyo serikali imekusudia kuwapatia.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni wa (JKT) Luteni Kanali Zakaria Kitani, aliwaasa wahitimu hao, kuhakikisha wanazingatia kiapo walichoapa kwa kuishi kwa utiifu na uadilifu siku zote sanjari na kutumia ujuzi waliofundishwa kuleta tija katika jamii kokote waendako.