December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliobomolewa Kipunguni kuanza kulipwa fidia Mwaka huu

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

WAZIRI wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewahakikishia wananchi wa Mtaa wa Kipunguni, uliopo katika Kata ya Kipawa, Jimbo la Segerea Jijini Dar es salaam, kuanza kulipwa fidia ya fedha zao Mwezi Agosti 2024, baada ya kubomolewa ili kupisha upanuzi wa uwanja cha ndege wa kimataifa wa JNIA .

Kauli hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, kumuomba, Katibu wa NEC, Itakadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, kushughulikia tatizo hilo la takribani zaidi ya miaka sita.

Waziri Nchemba akijibu changamoto hiyo kwa njia ya Simu, baada ya kupigiwa na Mwenezi Makalla, katikati ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Liwiti, iliyopo katika Jimbo la Segerea Wilaya ya Ilala, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuahidi hadi Agosti 2024 kuwa wakazi hao wataanza kulipwa.

“Ni kweli tatizo hilo nalifahamu na Mh Mbunge Bonnah amekuwa akifuatilia mara nyingi siwezi kuhesabau, lakini ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Katibu Mwenezi kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na hadi ifukapo mwezi Agosti mwaka huu wataanza kulipwa”, Amesema Nchemba kwa njia ya simu.

Aidha, amewaomba radhi wananchi hao kwa kuchelewa kulipwa fidia zao huku akisema Sababu ya kuchelewa ni changamoto zilizojitokeza Katika mwaka wa fedha uliopita ikiwemo Mafuriko ya Rujiji pamoja na kukatika kwa baadhi ya Barabara nchini kutoka na mvua za masika.

Amebainisha kuwa wataanza kuunganisha mifumo ya kifedha na Agosti 2024 kuanza hatua ya kulipa fidia kwa wananchi hao.