December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu wanaovaa mavazi yasiyo na maadili kurudishwa nyumbani

Na Richard Mwaikenda,TimesMajira Online,Dodoma

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewaagiza wakuu wa Shule za Sekondari kuwarudisha nyumbani walimu wanaokiuka maadili kwa kuvaa mavazi yasiyofaa shuleni.

Agizo hilo amelitoa Alhamisi wiki iliyopita alipokuwa akizungumzia umuhimu wa wakuu wa shule kudumisha nidhamu yao, wanafunzi na walimu katika shule wanazoziongoza ikiwa ni sehemu ya kulinda maadili na uzalendo.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo alipokuwa akihutubia wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), jijini Dodoma hivi karibuni.

“Nidhamu mliyonayo wakuu wa shule, iwe hivyo hata kwa walimu na wanafunzi. Msiogope walimu wachache wawe wanawaharibia sifa, asiyevaa vizuri msiogope kumrudisha nyumbani,” amesema Ndalichako.

Awali, Waziri Ndalichako amewasifu wakuu wa shule kwa nidhamu waliyonayo na jinsi walivyopendeza kwa kuvaa mavazi mazuri na ya heshima.

Amewataka pia kudumisha nidhamu kwa wanafunzi na kwamba wasiruhusu mila na desturi na maadili yakamong’onyoka, bali wawafundishe kuhusu nidhamu, uaminifu na uzalendo.

Amesema jambo hilo hata Rais Jamhuri ya Muungano, John Magufuli amelisisitiza wakati anawaapisha mawaziri na manaibu waziri Ikulu, Chamwino, Dodoma, kwa kuwataka wanafunzi kufundishwa somo la historia ya nchi ili kudumisha uzalendo.