November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu wakuu 4500 kupatiwa mafunzo ya uongozi wa Elimu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Uongozi bora, usimamizi na uendeshaji wa elimu ulio mzuri una mchango mkubwa katika maendeleo ya shule na elimu kwa ujumla.

Hayo yamesemwa wilayani Bagamoyo, Mkoa Pwani na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo katika uzinduzi wa kitaifa wa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa Shule kwa walimu wakuu wa Shule za Msingi nchini.

Amesema kwa sasa Serikali inaendelea na mabadiliko makubwa katika Sekta ya elimu ikiwemo kuhuisha Sera ya elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala hivyo suala la uongozi wa elimu katika rasimu hiyo ya sera limepewa kipaumbele.

“ADEM katika mabadiliko hayo mna wajibu mkubwa kusaidia Serikali kufikia malengo kwa kutoa mafunzo yatakayowajengea uwezo viongozi wa elimu katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupanga mipango kimkakati, usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, utawala bora usimamizi wa rasilimali, miiko na maadili ya kazi, ulinzi, haki na usalama wa watoto na huduma kwa mteja kama kushughulikia malalamiko kwa wakati “amesema Prof. Nombo

Akizungumzia mafunzo yanayofanyika amesema ni utekelezaji wa Mradi wa BOOST kupitia afua yenye lengo la kuimarisha usimamizi na utawala bora katika utoaji wa elimu ngazi ya shule katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Zaidi ya Sh Bilioni tatu zitatumika kutoa mafunzo kwa walimu wakuu zaidi ya 4500 katika awamu ya kwanza kutoka mikoa saba.

“Kwa sasa tumeanza na mikoa saba kwa idadi hyo ya walimu zaidi ya 4500, lengo la Serikali ni kutoa mafunzo kwa walimu wakuu wapatao 17,891,”amesema Prof. Nombo

Ametaja mikoa ambayo mafunzo yanatolewa katika awamu ya kwanza kuwa ni Pwani, Dar es Salaam, Njombe, Songwe, Morogoro, Dodoma na Mara

Ametoa wito kwa viongozi wa elimu wanaopata mafunzo hayo kuwa makini na wadadisi ili kuongeza umahiri utakaowezeshwa kusimamia uendeshaji wa shule kwa ufanisi.

“Baada ya mafunzo haya mkaendelee kuongoza shule kwa misingi ya utawala bora, simamieni miradi kwa uaminifu, zingatieni sheria za manunuzi na matumizi ya fedha,”amesema Prof. Nombo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Siston Masanja amesema mafunzo yoyote yanapotolewa yanalenga kutoa ujuzi, maarifa na kubadilisha mitizamo hivyo amewaomba walimu wakuu kupitia mafunzo hayo yenye lengo la kuimarisha usimamizi na utawala bora katika utoaji wa elimu yakawe chachu ya kuleta mabadiliko ya kiufanisi katika utendaji.