November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walengwa 400,000 Mpango wa TASAF waaga umaskini

*Wammwagia sifa Rais Samia kwa kuwawezesha kujimudu kimaisha waanzisha miradi, wajenga makazi, wasema wapo tayari kupisha wengine,

Na Reuben Kagaruki,Timesmajiraonline,Arusha

WALENGWA 400,000 wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezWa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wataondolewa kwenye mpango huo baada ya kujimudu kimaisha wakiwa wameanzisha miradi ya kuwaingizia kipato pamoja na kujenga makazi bora ikilinganishwa na huko nyuma.

Kutokana na mafanikio hayo walengwa waliozungumza na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro wiki iliyopita walikiri hali zao za maisha kuboreka na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza Mpango huo, ambao umewatoa kwenye umaskini na kwamba sasa wapo tayari kuondoka ili kupisha wengine waweze kunufaika kama wao.

Idadi ya walegwa 400,000 wanaotarajiwa kuondolewa kwenye mpango huo baada ya kujimudu imetangazwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Shedrack Mziray, wakati akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Arusha.

Mziray alisema kwa sasa tayari wameishafanya tathmini ambapo wamebaini wana walengwa 400,000 ambao sasa wanaweza kujimudi kimaisha na wanaweza kutoka katika mpango .

“Nia yetu ni kuziondoa kaya kwenye hali ya umaskini uliokithiri na baadaye ziweze kujimudu kimaisha. Tathimini yetu inaonesha walengwa 400,000 wanatakiwa kuondolewa,” amesema Mziray na kuongeza;

“Utaratibu unatutaka tunapozitambua hizi kaya na kuziingia kwenye mpango na kuanza kuzihudumia baada kipindi fulani zifanywe tathmini
ili zile kaya ambazo zimeboreka kimaisha ziweze kuondoka na kupisha kaya nyingine.”

Hata hivyo, Mziray amesema eneo hilo ndipo kunakuwa na ugumu, kwani mtu akishazoea kupata kitu fulani hasa kupewa ruzuku, halafu akiambiwa ruzuku imesimama na kutakiwa kuendelea na maisha ya kawaida, kidogo kunakuwa na changamoto.

“Lakini huo ndiyo utaratibu na tunapoingiza kaya siku ya kwanza kwenye mpango tunawambia wahusika wanaingia kwenye mpango huo, lakini baada ya kujimudu wataondolewa,” amesema Mziray.

Hata hivyo, amesema kuna aina ya kaya wanazoziingiza hata wakae nazo milelele haziwezi kutoka kwenye umaskini kutokana na uhalisia wa hizo kaya.

Ametolea mfano wazee sana, akisema hautegemei hao wakishapata ruzuku waanzishe miradi waweze kuiendesha na wakatoka kwenye kiwango fulani cha umaskini ,wakaweza kuendesha shughuli zao.

“Kwa hiyo watu wa namna hii wakiingia kwenye mpango hata ukae nao muda gani hauwezi kuwatathimini na kuona wametoka kwenye umaskini, kwa hiyo hao lazima tuendelee nao,” amesema.

Alisema watu kama hao kwenye nchi za wenzetu wamekuwa wakiingizwa kwenye pensheni na Zanzibar wanapata ruzuku ya kila mwezi hadi maisha yao yatakapokwisha.

“Kwa hiyo hata kwenye mpango tuna watu wa namna hiyo ambao hatutegemei kwamba watahitimu, hao tutaendelea kuwa nao, lakini kuna watu tayari wameanza kujimudu hao tunawaondoa,” amesema Mziray na kuongeza;

“Kwa hao, ndiyo tunafanya tathmini na tukiwabaini kwamba wamevuka kile kiwango tulichokiweka mwanzoni cha umaskini, basi huwa tunawapa taarifa na kuwatoa kwenye mpango.”

Amesema kwa jinsi wanavyoanza kutekeleza uamuzi huo inawezekana yakasikika maneno maneno, lakini wataondolewa kwa sababu wana uwezo kuliko wengine ambao hawako kwenye mpango.

“Zoezi hili tunalifanya katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, na unajua na wananchi kikifika kipindi cha uchaguzi na wenyewe wanakanyagia chini,” amesema .

Wakizungumzia uamuzi huo wa TASAF, baadhi ya walengwa walimpongeza Rais Samia kwa kuwaondoa kwenye umaskini na kwamba wanastahili kuondolewa kwa sababu wanajimudu tena kuliko wale ambao hawapo kwenye mpango kwa sasa.

“Kwa kweli tunamshukuru Rais Samia kwa kuendeleza mpango huu, ameweza kutuondoa kwenye umasikini. Ninaweza kujimudu nipo tayari kuondolewa kwa hiari yangu ili nipishe wengine,” amesema mlengwa wa TASAF, Valeria Teti (56) mkazi wa Kata ya Boma Mbuzi, Mtaa wa Relini Halmashauri ya Manispaa Moshi na kuongeza;

“Wengine tukiambizana tuombe tuondolewe kwenye mpango kwa sababu tunajimudu, wanasema tusiseme, lakini ukweli ni kwamba kwa sasa tunaojimudu.”

Kwa upande wake Shuvaa Hassan (56) Mkazi wa Kata ya Kaloleni, Mtaa Kilimani Manispaa ya Moshi, alisema hata sasa akiambiwa aondolewe TASAF yuko tayari, kwani ana biashara zake ambazo zinamuingizia kipato cha kati ya sh. 40,000 hadi 50,000 kwa siku.

“Nipo tayari kuondolewa TASAF ili wengine waingie nina duka langu linaniingizia kipato, kwa kweli tunamshukuru sana Rais Samia,” amesema Hassan.

Naye Fredelina Swai, amesema hana cha kumueleza Rais Samia kwa sababu TASAF imesomesha watoto wake wawili na sasa wapo vyuo vikuu. Alisema amejiandaa kuondoka kwenye mpango huo kwa sababu ameanzisha miradi yake ambayo inamuingizia kipato.