Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali,Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote nchini ambao bado hawajakamilisha kuteua wajumbe wawili wa Kamati za ushauri wa kisheria ngazi za mikoa na wilaya kwa mujibu wa mwongozo wa huduma za ushauri wa kisheria za mikoa na wilaya kifanya hivyo ili kamati hizo zianze kazi ya kusikiliza malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa.
Jaji Feleshi amesema hayo jijini hapa leo,Juni 26,2024 wakati akizindua Kliniki ya ushauri na Elimu ya kisheria kwa umma ambapo amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo mshauri mkuu wa Serikali katika masuala yote ya kisheria .
“Ibara ya 8(1)(a)ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza kwamba Mamlaka yote katika nchi yatatoka kwa wananchi,pia ibara ya 8(1)(b)-(c) ya katiba hiyo inatamka bayana kuwa lengo la msingi la serikali litakuwa kushughulikia masuala ya wananchi na kwamba Serikali itawajibika kwa wananchi wake,”amesema Jaji Feleshi.
Ameeleza kuwa Kliniki hiyo ni matokeo ya wajibu wa kikatiba unaoitaka serikali kuwajibika katika masuala ya wananchi wake.
“Hivyo kwakuwa serikali inawekwa madarakani na watu,serikali kupitia Ofisi yangu inao wajibu wa kushughulikia masuala ya wananchi,”amesema.
Aidha ameeleza kuwa kiliniki hiyo ni mwanzo wa mpango kabambe wa serikali wa kutoa huduma za msaada wa kisheria nchini katika maeneo ya Mijini na Vijijini.
“Kliniki hii ya msaada na elimu ya kisheria kwa umma inakusudia kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu na wananchi na kufikia malengo,
“Ambayo ni kutekeleza maagizo ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara kwa viongozi wa serikali kuweka utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatatua ikiwa ni pamoja na kuwaongoza katika taratibu za kupata haki zao pale zinapovunjwa au zinapoonekana kuelekea kuvunjwa,”amesema Jaji Feleshi.
Vilevile kupunguza migogoro dhidi ya Serikali kwani wananchi wakisikilizwa na kupata suluhu ya changamoto zao za kisheria dhidi ya serikali,hawatakuwa na haja ya kuishtaki serikali katika vyombo mbalimbali vya utatuzi wa migogoro nje na ndani ya nchi.
Pia kudumisha utawala bora kwakuimarisha utawala wa sheria nchini,kuongeza Utengamao na utulivu katika jamii na kuchochea maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla na kuboresha mazingira na kuongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Pamoja na hayo ametoa rai kwa Mawakili wote wa serikali hapa nchini kutenga muda na kuwasikiliza wananchi katika maeneo yao kupitia kamati za ushauri wa kisheria ngazi za mikoa na wilaya zilizozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa katika mkutano wa chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Dodoma,Machi 21,2024.
“Navikumbusha Chama cha Mawakili wa Serikali(TPBA) pamoja na Chama cha Mawakili wa Tanganyika(TLS) kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na kamati za ushauri wa kisheria ngazi za mikoa na wilaya ili kusikiliza malalamiko ya wananchi,
“Kliniki zitakazoendeshwa na kamati hizo zitakuwa enedelevu kwa nchi nzima ambapo mawakili wa serikali na wadau katika utaoaji wa msaada wa kisheria watatoa huduma katika maeneo yao,”amesema Jaji Feleshi.
Naye Makamu wa rais wa chama cha Mawakili wa serikali Tanzania Ellen Rwijage, alitoa wito kwa watanzania wote wenye kero zinazohusu masuala ya sheria kujitokeza kupata huduma hiyo bure.
Hata hivyo,amesema mawakili wa serikali wamejipanga kutoa huduma kwa muda wa wiki moja ambao utatumika kusikiliza na kutoa elimu na ushauri wa kisheria.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote