December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wapewa mbinu za kuinuka kiuchumi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKULIMA na wafugaji wa Mikoa ya Tabora na Kigoma wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazoletwa na serikali ya awamu ya 6 na kutumia teknolojia ya zana bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao yao.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali wa Polisi Mstaafu Thobias Andengenye alipokuwa akihutubia wakazi wa Mikoa ya Kigoma na Tabora katika kilele cha maonesho ya sikukuu ya wakulima nane nane Kanda ya Magharibi yaliyohitimishwa jana katika viwanja vya Ipuli Mjini Tabora.

Aliwataka wazalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kutoka katika Mikoa hiyo kutumia teknolojia ya zana bora na mbegu bora za mazao na mifugo ili kuongeza uzalishaji wa mazao mengi zaidi na shughuli zao kuwa na tija kubwa.

Alipongeza mwitikio mkubwa wa wakulima, wafugaji, wavuvi na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali vilivyojitokeza kushiriki maonesho hayo kutoka ndani na nje ya Mikoa hiyo ili kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali wanazotoa.

RC aliwataka kutumia elimu, ujuzi, teknolojia na maarifa waliyopata kupitia maonesho hayo ili kukuza shughuli zao za kilimo, mifugo na uvuvi katika maeneo yao na kuongeza kuwa maonesho hayo ni fursa muhimu sana kwao.

‘Tunampongeza sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake njema ya kuinua maisha ya wakulima na wafugaji nchini kupitia programu mbalimbali ikiwemo kuboresha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi’, alisema.

Alitaja baadhi ya programu zilizoanzishwa na Mheshimiwa Rais kuwa ni Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ambapo vijana 812 wanapatiwa mafunzo ya kilimo biashara kupitia programu hii na muda si mrefu watahitimu.

Program nyingine ni Uanzishwaji wa Majukwaa ya uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambapo watawezeshwa mitaji (mikopo), ruzuku, kutafutiwa masoko na uboreshwaji miundombinu ya kiuchumi, aliagiza halmashauri zote kuhakikisha majukwaa haya yanafanya kazi.

Alitaja mikakati mingine ya serikali kuwa ni kuongeza Bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka sh bil 751.1 mwaka 2022/2023 hadi bil 970.7 mwaka 2023/2024 na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka bil 176.2 mwaka 2022/2023 hadi bil 295.9 mwaka 2023/2024 ili kuimarisha huduma za ugani na miundombinu muhimu itakayochochea ukuaji wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Aidha katika miradi ya kimkakati alisema ujenzi wa barabara za lami zinazounganisha mikoa hiyo 2 ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR inayoendelea kutekelezwa, kipande cha km 294 cha Makutupora-Tabora na km 506 Tabora-Kigoma itachochea kwa kiasi kikubwa uchumi wa Mikoa hiyo.

RC Andengenye alipongeza vikundi vyote vinavyojishughulisha na uzalishaji bidhaa za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kutoka katika halmashauri zote 16 za Mikoa ya Kigoma na Tabora kwa kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo.

Aliwataka Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa Mikoa ya Kigoma na Tabora na wote wanaohusika kuratibu maonesho haya Kuandaa mpango mahususi wa matumizi ya uwanja huo, ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi. Aidha aliwataka kuendelea kuboresha mabanda yao ili yaweze kukidhi hadhi ya maonesho ya kitaifa na kimataifa na kusisitiza ambapo aliagiza ujenzi wa mabanda hayo kukamilika haraka na kuwa ya kudumu.

Aidha RC Andengenye aliwataka kutumia fursa za masoko zilizoko katika nchi jirani za DRC Congo, Burundi, Rwanda na Zambia ili kumaliza changamoto ya masoko ya bidhaa zao.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu Thobias Andengenye akihutubia wananchi kwenye kilele cha Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane Kanda ya Magharibi iliyofanyika ktk viwanja vya Ipuli mjini Tabora.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi akitoa salamu ktk maonesho ya wakulima nane nane
Mkulima kutoka Mkoani Kigoma akionesha shamba lake la nyama lililostawi sana alilolima mwaka huu kwa kufuata kanuni za kilimo bora.