Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Morogoro
WAKAULIMA kwenye skimu za kilimo cha umwagiliaji Mvumi, Msolwa, Ujamaa na Njage zilizopo katika Wilaya za Kilosa, Kilombero na Halmashauri ya Mlimba mkoani Morogoro, zimenufaika na kukamilika kwa ujenzi wa skimu za kilimo cha umwagiliaji zilizopo chini ya mradi wa kuongeza uzalishaji wazao la mpunga uliofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Wakizungumza kwa tofauti, baadhi ya wakulima katika skimu hizo wamesema hali ya kilimo katika skimu hizo haikuwa rafiki kabla ya kuwepo kwa ujenzi wa miundombinu hiyo ambapo kwa sasa, hali ya kilimo ni nzuri kwani kuna uhakika wa kupata wastani wa mavuno ya magunia 20 mpaka 30 kwa heka kutokana na uhakika na matumizi sahihi ya maji katika misimu tofauti ya kilimo.
Mmoja wa wakulima katika Skimu ya Mvumi, Mwanaisha Kaluwa amesema; “Naishukuru serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kwa kutuletea mradi wenye manufaa kwetu sisi wakulima, lakini ombi langu ni kwamba serikali itutafutie masoko ya uhakika, kwani kwa sasa tunauza kupitia madalali ambao wanatuumiza sana, hawatumii vifungashio halali wanafunga kwa kutumia rumbesa, tunaomba serikali isimamie mpunga uuzwe kwa kutumia mizani”.
Kwa upande wake Ofisa Kilimo Halmashauri ya Mlimba, Wadara Kidata akizungumzia skimu ya kilimo cha umwagiliaji Njage amesema, kabla ya mradi huo ilikuwa na changamoto ya maji ambayo kwa sasa wanapata maji kwa wakati, barabara nzuri ambazo zinarahisisha mazao kufika ghalani kwa wanunuzi kwa wakati na gharama nafuu.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mhandisi wa Mkoa wa Umwagiliaji Morogoro, Njanji Mlole amesema kabla ya kukabidhi mradi huo ambao upo katika muda w amatazamio, upungufu mchache ulijitokeza ikiwa ni pamoja na kurekebisha mabanio na kuinua sehemu ya vipange vya barabara za skimu na kubadilisha makaravati katika Skimu ya Njage Mlimba na kuingiza mfumo wa majisafi katika vyoo, yatarekebishwa katika kipindi hicho kwa mujibu wa mkataba.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi