Na Joyce Kasiki,Timesmajira onine,Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzaia (TSB) Saddy Kambona amesema Bodi hiyo imeendelea kuhamasisha wakulima wadogo kufanya kilimo cha zao la mkonge kwani kina tija kubwa huku akisema,bodi hiyo inakodisha mashamba ya zao hilo kwa wakulima hao wadogo .
Saddy ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TSB kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 huku akisema lengo la kukodisha mashamba hayo ni kuwasaidia wakulima wadogo waweze kulima zao hilo.
Mkonge ulikuwa unalimwa na wakulima wakubwa pekee waliokuwa wanamiliki mashamba makubwa, hakukuwa na wakulima wadogo wa mkonge, uzalishaji wa mkonge uliongezeka mwaka hadi mwaka na hadi kufikia mwaka 1964 Tanzania iliweza kuzalisha takriban Tani 230,000 na kuongoza Duniani kwa uzalishaji wa zao la mkonge.
Kipindi hicho Mkonge ulikuwa unachangia takriban 65% ya fedha za kigeni nchini kabla ya uzalishaji kuanza kuporomoka kuanzia mwaka 1970 ambapo hadi kufikia Mwaka 1997 uzalishaji wa Mkonge kwa Mwaka ulikuwa ni tani 19,000 tu.
Kufuatia hatua hiyo ya uhamasishaji na ukodishaji mashamba kwa wakulima wadogo, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la wakulima wadogo ambapo hadi mwaka 2020 TSB iliweza kusajili wakulima wadogo 6,887 na kwamba Mwaka 2022 idadi ya wakulima wadogo waliosajiliwa walikuwa ni 8,972.
“Pamoja na kuwa na idadi hiyo ya wakulima wadogo lakini pia wapo wakulima wadogo wa Mkonge ambao hawajafikiwa na kusajiliwa na TSB wanaokadiriwa kufikia 22,000,na hii ni kutokana na hamasa kubwa ya kilimo cha Mkonge iliyofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais Tamisemi kupitia Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Bunge na Bodi ya Mkonge Tanzania.”amesema Saddy na kuongeza kuwa
” TSB imegawa mashamba kwa wakulima 983 Wilayani Korogwe na wakulima wengine zaidi ya 3,000 wamegawiwa mashamba Wilayani Kilosa na zoezi bado linaendelea,hii ni baada ya Mheshimiwa Rais kufuta mashamba pori Wilayani Kilosa, Morogoro na kuiongezea mashamba TSB kwa ajili ya kuwagawia wakulima wadogo walio tayari kulima mkonge pamoja na kushusha riba kwenye mabenki ya biashara kwa mikopo inayoelekezwa kwenye kilimo na hivyo kuleta unafuu mkubwa sana kwa wakulima.”
Mkurugenzi huyo amesema bodi imefanikiwa kununua mitambo mipya ya kuchakata Mkonge na kufufua mitambo ya kuchakata Mkonge ya Mashamba ya Kibaranga Wilayani Muheza, Tanga na shamba la Serikali la TPL lililopo Kata ya Bwawani Wilayani Arumeru, Arusha ambalo linasimamiwa na kuendeshwa na TSB.
“Mitambo hii itasaidia sana kuongeza uzalishaji wa Mkonge na hivyo kuwezesha kufikiwa kwa lengo la uzalishaji lililowekwa na Serikali,hii inaonesha kwamba Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuimarisha kilimo na kuhakikisha kuwa kilimo kinakua kufikia asilimia 10 ifikapo Mwaka 2030 (Agenda 10/30 kilimo ni biashara.”amesisitiza
Aidha amesema,kuanzia mwaka 2018, Serikali iliamua kuchukua hatua za makusudi za kufufua zao la Mkonge na kuifufua na kuijenga upya Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, 2019 Serikali ililiingiza zao la mkonge katika orodha ya mazao ya kimkakati na kufanya zao hilo kuwa zao la saba la kimkakati huku mazao mengine ya kimkakati ni pamoja na Pamba, Tumbaku, Kahawa, Korosho, Chai, Michikichi.
Vile vile amesema,zao la Mkonge likaingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025 ambamo limewekwa lengo la kuongeza uzalishaji kutoka tani 36,000 zilizokuwa zinazalishwa kwa Mwaka 2020 hadi kufikia tani 80,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025.
“Serikali ikaongeza lengo na kuiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 kwa mwaka, ifikapo mwaka 2025/2026”amesema na kuongeza kuwa
“Hatua za Serikali kuliingiza zao la mkonge kwenye orodha ya mazao ya kimkakati ilitokana na ukweli kwamba mahitaji na soko la mkonge limezidi kuimarika duniani,hii ni kutokana kugundulika kwa matumizi mapya ya mkonge na uzalishaji wa bidhaa mpya zitokanazo na mkonge kama vile vifaa vya ujenzi(gypsum boards, Matofali,mbao, mabati, vigae), Sukari ya Mkonge, Pombe ya Mkonge, Karatasi maalum, Bio Gas, mbolea, Chakula cha mifugo , urembo, mabodi ya magari “Amesema Saddy
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea