October 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wa mazao ya Jamii ya mikunde Shinyanga wakumbuka Mfumo wa Stakabadhi za Ghala

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga

BAADHI ya wakulima wa mazao ya jamii ya mikunde mkoani Shinyanga wamelalamikia kitendo cha kuporomoka kwa bei ya zao la choroko tofauti na ilivyokuwa msimu wa mwaka uliopita wakati zao hilo liliponunuliwa kwa mfumo wa Stakabadhi za ghala.

Malalamiko ya wakulima hao yanatokana na wanunuzi binafsi wa choroko hivi sasa kununua zao hilo kwa bei kati ya shilingi 800.00 na 900.00 kwa kila kilo moja tofauti na mwaka uliopita ambapo kupitia mfumo wa Stakabadhi za ghala waliuza kwa bei ya shilingi 1,200.00 mpaka 1,300.00 kwa kilo moja.

Wakizungumza na mwandishi wa Times Majira Online mjini Shinyanga wakulima hao wameelezea kusikitishwa na hatua ya wanunuzi kutoa bei ndogo tofauti na ahadi zao za hapo awali waliposhinikiza mazao ya jamii mikunde yasiuzwe kwa mfumo wa Stakabadhi za ghala.

Stephen Masanja na Mawemilu Charles wakazi wa kata ya Uchunga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamesema wamesikitishwa na bei inayotolewa na wanunuzi hivi sasa ambayo ni ya chini ikilinganishwa na bei waliyokuwa wakiuza kwa njia ya minada misimu iliyopita.

“Kwa kweli hii bei ya inayotolewa hivi sasa inasikitisha, mwanzo tuliamini hawa wanunuzi binafsi watakuwa na bei nzuri kama walivyokuwa wakidai mara baada ya Serikali kuruhusu choroko na dengu ziuzwe kwa mfumo wa Stakabadhi za ghala, lakini mfumo huo waliupinga na ukafutwa,”

“Hawa wanunuzi binafsi walidai kwa kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala ulikuwa ukiwapunja wakulima kutokana na kutoa bei ndogo, hivyo Serikali iliagiza mfumo huo usitumike, na kila mnunuzi aruhusiwe kwenda moja kwa moja kwa wakulima kununua mazao hayo, tuliamini bei itakuwa nzuri, kumbe sivyo kabisa,” anaeleza mmoja wa wakulima hao.

Wakulima hao wameendelea kueleza kuwa awali msimu wa uuzaji wa choroko ulipoanza wanunuzi walitoa bei ya shilingi 1,000.00 lakini hivi sasa bei hiyo imeshuka na kufikia shilingi 800.00 hadi 700.00 kwa kila kilo moja bei ambayo wanadai ni ndogo na haiwarejeshei gharama wanazotumia kwenye kilimo.

“Kuna timu iliundwa na aliyekuwa waziri wa kilimo Profesa Adolf Mkenda mwaka juzi, Septemba 2021 kuchunguza na kukusanya maoni kutoka kwa wakulima na wadau wa kilimo kuona iwapo mfumo wa uuzaji mazao kwa mfumo wa stakabadhi za ghala una maslahi kwa mkulima ama laa,”

“Jambo la kusikitisha leo hii ni takribani mwaka mmoja na nusu Serikali haijaleta majibu ya kitu gani walichokipata kutoka kwenye timu iliyoundwa ambayo iliongozwa na Dkt. Hamis Mwinyimvua na katibu wake akiwa Ernest Doriye, tunaomba basi angalao tujue matokeo ya kazi ya timu hiyo,” anahoji Lucas Charles.

Wakulima hao wameiomba Serikali kupitia wizara yake ya kilimo kuangalia upya maamuzi yake ya kuzuia kutumika kwa mfumo wa Stakabadhi za ghala katika kuuza mazao ya jamii ya mikunde na kwamba mfumo huo ni mzuri na unalinda bei ya mazao ya mkulima tofauti na bei ya wanunuzi binafsi.

“Mfumo wa Stakabadhi za ghala ni mfumo mzuri katika suala zima la uuzaji wa mazao ya wakulima iwapo tu Serikali itausimamia na kuhakikisha mazao yote yanauzwa kwa njia ya mnada, maana ni mfumo huru na unaruhusu kila mnunuzi kushindanisha bei kwenye mnada badala ya hali ilivyo sasa,” anaeleza Lucas.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Shinyanga (SHIRECU), Kwiyolecha Nkilijiwa anasema kuporomoka kwa bei ya mazao ya jamii ya mikunde kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali kutokuweka mkazo kwenye uuzwaji wa mazao hayo kwa njia ya minada.

“Binafsi naamini na nitaendelea kuamini Mfumo wa Stakabadhi za ghala ndiyo mfumo wenye faida na sahihi wa uuzaji wa mazao yote ya wakulima hapa nchini, hawa wanaoupinga mara nyingi hufanya hivyo kwa kulinda maslahi yao binafsi, na ushahidi ni huu tunaouona hivi sasa,” anaeleza Nkilijiwa.

Baadhi ya wakulima wa zao la choroko wilayani Kishapu wakipima choroko zao katika Chama chao cha msingi (Amcos) wilayani Kishapu.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) Mkoani Shinyanga, Kwiyolecha Nkilijiwa.
Zao la Choroko katika picha.
Waziri wa kilimo Hussei Bashe.