Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
IMELEEZWA kuwa wakulima wa zao la kahawa wamekuwa wakishindwa kuzalisha kwa tija kutokana na kutopima afya ya udongo ili waweze kujua ni mbolea gani inafaa na badala yake wamekuwa wakifanya kilimo cha mazoea na wengine kutojua jinsi ya kuzuia magonjwa ya kahawa ,kutojua staili za kisasa za ukataji .
Kauli hiyo imetolewa jana Msimamizi mkuu wa shamba la kahawa Utengule Coffe ,Amani Ngowi wakati wa siku ya mkulima ambapo wakulima mbali mbali walifika katika shamba hilo kupata kanuni bora za kilimo cha kahawa kutoka kwa watalaam wa kilimo .
Ngowi amesema kuwa alichobaini ni kwamba wakulima wanashindwa kuzalisha kahawa kwa wingi kutokana na kutopima udongo ,kutokujua mbolea gani inahitajika na kufanya kilimo cha mazoea na wengine kutojua jinsi ya kuzuia magonjwa ya kahawa mashambani .
“Kuna magonjwa mengi yanatokea kwenye kahawa lakini wakulima wengi hawafahamu mfano mwaka jana ugonjwa wa hawa wadudu wadogo wadogo walitokea mwaka jana lakini wakulima hawafahamu ,tunashauri wakulima wapate elimu juu ya kilimo cha kisasa pia serikali iwasaidie wakulima wapate mbegu bora za kahawa hii changamoto kubwa sana na hii itawasaidia wataweza kujikwamua kwenye kilimo mazoea na kwenda kilimo cha biashara”amesema Msimamizi huyo wa shamba .
Upendo Sailosi ni Mkulima kutoka utengule amesema kuwa kwenye kahawa kuna changamoto nyingi ambazo huwa wanatamani zitatuliwe lakini wakati mwingine zinatuliwa kiasi na zingine hazitatuliwi hasa kwenye Kahawa ambapo kuna wadudu ambao wanatoboa kwenye miti ya kahawa kahawa haiwezi kustawi tena na mti huoza.
Mkulima huyo amesema kuwa siku ya mkulima huwa inakuwa msaada mkubwa kwani kwani kuna mafunzo ambayo huwa yanatolewa ambayo yana tija kwa mkulima ambapo hujifunza vitu ambavyo havijui na kumwongezea maarifa zaidi katika shughuli zake za kilimo .
Mkulima mwingine wa Utengule Usongwe Peter Mwashitete amesema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia namna ya kuotesha mbegu kisasa na kupeleka shambani namna ya kukata miti ya kahawa pamoja na uchumaji mpaka kuvundika .
Mwashitete amesema kwamba Bodi ya Kahawa imewasaidia kupata mafunzo na usimamiaji mzuri wa zao kahawa Tanzania , ubora wa kahawa , minada ,bei ya kahawa hivyo kwa wakulima msaada mkubwa sana.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mbeya bodi ya Kahawa (TCB)Sijali Boa amesema kuwa lengo kubwa la siku ya mkulima ni kuwaleta wakulima na wadau wengine kuwafundisha mbinu mbali mbali za kilimo cha kahawa ambapo mwisho wa siku tunategemea wakizifuata wazalishe kwa tija na kuongeza uzalishaji .
Boa amesema kuwa wamechagua shamba hilo kubwa la Kahawa la Utengule ili kuonyesha kuwa wenzao wanafuata hatua zote za kilimo cha kahawa na wanazalisha kwa tija na kwa wingi lengo kubwa ni katika kuonyesha utofauti na kwamba wakulima wadogo wadogo waliopo pembeni mwa shamba wanalima na kufuata mbinu bora za kilimo cha kahawa lakini hawazingatii kwa kiwango kinachotakiwa hivyo kushindwa kuzalisha kwa wingi .
Aidha amesema kuwa matarajio yao baada ya mafunzo hayo ni kuwataka wakulima kufuata mbinu bora za kilimo ili waweze kuzalisha kwa tija na kupata kipato kikubwa zaidi.
“Pia tunatoa elimu kuhusiana na masuala ya afya ya udongo kimsingi unapokwenda kuzalisha sehemu yeyote lazima upime afya ya udongo kwanza ili kujua udongo uliopo kwenye mashamba yao unahitaji aina gani ya mbolea hii itawafanya wakulima kujua aina ya udongo uliopo kwenye mashamba yao na kufahamu aina ya mbolea inayofaa kutumiwa”amesema Meneja huyo wa Kanda.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi