January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima tumieni teknolojia mpya ya kuchakata viungo na matunda

Na Mwandishi wetu, timesmajira, Online

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),imewataka wakulima wanaochakata matunda na viungo kuanza kutumia teknolojia mpya ya mashine ya kuchakata matunda na viungo hivyo na kufanya kuwa katika mfumo wa unga ili kumsaidia mkulima kuhifadhi mazao yasiharibike kwa muda mrefu.

Akizungumza jana kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam,katika banda la VETA,mbunifu wa mashine hizo George Nyahende amesema mashine hiyo ni nyenzo bora ya kisasa inayomsaidia mkulima hata mjasiriamali kuchakata mazao na kuyaongezea thamani.

Nyahende amesema mashine hiyo ina sehemu tatu ambazo kila moja ina kazi yake.Moja ni ya kukatakata viungo au matunda tayari kwa kuyakausha kwenye machine nyingine ndogo na baada ya hapo inaingia kwenye mashine ya kusaga kuwa unga.

“Huu ni ubunifu mpya, niliona wakulima hususani vijijini wanapata hasara ya mazao yao mfano vitunguu wanavuna wakati mwingine soko halipo vinaharibika,sasa wakitumia mashine hii wanavikausha vitunguu na kuvisaga kuwa unga na hapo unahifadhi kwa muda mrefu,”amesema Nyahende.

Alisema aliamua kubuni mashine hiyo kwa sababu hivi sasa maeneo mengi ya vijijini umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA),wamesambaza umeme maeneo mengi hivyo wakulima wengi wanaweza kununua mashine hiyo na kuondokana na umaskini

Amesema mashine hiyo sio mtu kwa mkulima bali pia kwa wajasiriamali wadogo wanaweza kufungua kiwanda kidogo nyumbani na kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na kukuza uchuni wao.

Amesema moja ya mashine hizo ambayo ni ya kukausha matunda,viungo au nyama hutumia muda kati ya saa sita hadi 12 kulingana na bidhaa na baada ya hapo unasaga na kupata unga kisha unaweza kuufungasha kwa ajili ya kuhifadhi.

Amewataka wajasiriamali na wananchi kutembelea banda la VETA katika maonesho hayo kujionea mashine hiyo ili kuelimishwa na kuinunua kwa sababu ina faida nyingi za kuongeza kipato .