December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima Tabora, Kigoma wanufaika na kilimo Cha mbogamboga

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

VIKUNDI vya wakulima kutoka Mikoa ya Tabora na Kigoma vimeanza kufurahia matunda ya kilimo cha mbogamboga na matunda baada ya kupata mafanikio makubwa kutokana na elimu ya kilimo bora waliyopata kutoka kwa wadau.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walieleza kuwa licha ya kujishughulisha na kilimo hicho kwa muda mrefu hawakupata mafanikio lakini baada ya kupewa elimu ya kilimo bora na kuanza kutumia mbegu bora sasa uchumi wao umeanza kuboreka.

Mkulima Zabron Batega (35) mkazi wa Tabora alisema kwa zaidi ya miaka 10 amekuwa akijishughulisha na kilimo cha mbogamboga pasipo kuwa na mwongozo wa wataalamu wala kutumia mbegu bora hivyo kushindwa kuinuka kiuchumi.

Aliongeza kuwa elimu waliyopata kutoka kwa mdau wa kilimo kampuni ya EAST-WEST SEED imekuwa kichocheo kikubwa cha mafanikio yao baada ya kuanza kulima kwa kufuata ushauri wa wataalamu na kupanda mbegu bora.

‘Mwaka jana nililima ekari moja ya nyanya na kupanda miche 1700 lakini sikupata mafanikio makubwa ila baada ya kupata elimu, kutumia mbegu bora na kuweka mbolea, nimelima robo eka tu na kupanda miche kidogo mwaka huu na kupata zaidi ya sh mil 9’, alisema.

Sostene William (40) mkulima mkazi wa Mkoa wa Kigoma alisema awali alikuwa analima kilimo cha mazoea pasipo kufuata kanuni za kilimo bora cha mboga mboga lakini baada ya kupata ushauri wa kitaaluma sasa amepata mafanikio.

Alibainisha kuwa miaka ya nyuma alikuwa akilima na kupanda miche 4000 ya nyanya ambapo alikuwa anavuna na kuuza kiasi cha sh mil 1 hadi 2 lakini mwaka huu amelima na kupanda miche hiyo hiyo na kuuza zaidi ya sh mil 18.

Mwakilishi wa Kampuni ya EAST-WEST SEED Kanda ya Magharibi Alpha Kisendi aliwataka wakulima wote kuchangamkia kilimo cha mboga mboga na matunda kwa kuwa kinalipa huku akisisitiza kuzingatiwa kanuni za kilimo bora.

Alitaja siri kubwa ya mafanikio ya wakulima kuwa ni kuzingatia ushauri wa wataalamu, kufuata kanuni na kutumia mbegu bora zilizothibitishwa na wataalamu wa kilimo.

Alibainisha kuwa kampuni hiyo imesaidia vikundi vingi sana vya wakulima katika Mikoa mbalimbali hapa nchini hivyo akatoa wito kwa jamii kufuata maelekezo ya wataalamu na kutumia mbegu bora za mboga na matunda ili kuinuka kiuchumi.

Afisa Kilimo na Mwakilishi wa Kampuni ya East-West Seed Kanda ya Magharibi Alpha Kisendi akionesha shamba la mmoja wa wakulima kutoka Mkoani Kigoma aliyenufaika na elimu ya kilimo bora iliyotolewa na Wataalamu wa Kampuni hiyo na kuwawezesha kupata mavuno mengi tofauti na miaka ya nyuma. Picha na Allan Vicent