Na Mwandishi Wetu, TimesMajira, Online Njombe
WAKULIMA na maofisa ugani wamehimiza wakulima waelimishwe kulinda afya ya udongo, huku wakisifu juhudi ambazo zinafanyika hivi sasa kukuza matumizi ya mbolea asilia ili kuinua tija katika sekta ya kilimo na kufanya kilimohai kuenee nchini kote.
Aidha, baadhi ya maofisa ugani wastaafu wameeleza kufurahishwa na bidii inaofanywa wakati huu kupambana na tindikali ardhini ambayo inachakaza ardhi na kupunguza sana mavuno.
Wakizungumzia mbolea ya kukuza kilimohai iliyozinduliwa majuzi mjini hapa, maofisa ugani wamesifu utengenezaji wa mbolea hiyo, lakini wamehimiza pia matumizi mbole zinazotokana na wanyama na mimea.
Ofisa ugani mstaafu, Florence Mapunda amesema kuna haja kubwa sasa ya kuwaelemisha wakulimu juu matumizi sahihi ya mbolea kwa sababu sasa hivi watu wengi wana elimu.
“Nyakati zetu nilipata shida kuwafundisha wakulima kwa sababu nilikuwa mwanamke. Watu walizoea bwana shamba. Tulikuwa na mashamba darasa na tuliwahimiza watu kutumia mbolea za wanyama na mimea iliyooza.
Mbolea huirudishia ardhi rutuba, lakini wakati huo pia watu walikuwa wachache,” ammesema
Amewaomba maofisa ugani wa sasa kuwafundisha wakulima juu ya afya ya udongo.
Ameeleza kwamba wakulima wengi hawajui kwamba matumizi ya muda mrefu ya mbolea za viwandani yanaharibu afya ya udongo hivyo fursa iliyojitokeza itumike kuwafundisha wakulima.
“Lazima tutumie mbole, lakini tuwe makini sana tunapotumia mbolea hizi ili kulinda afya ya udongo,” amesisitiza.
Afisa Mstaafu, Gerald Mhagama amependekeza vyuo vikuu, vyuo vya mafunzo ya kilimo na taasisi za utafiti na maofisa ugani wafanye juhudi ya pamoja kuwafundisha wakulima juu ya matumizi ya mbolea.
“Hawa watafiti wetu wanapopeleka matokeo yao kwa wakulima, basi wawafundishe namna ya kulinda afya ya udongo na matumizi mazuri ya mbolea.
Tunahitaji juhudi ya pamoja kukuza tija katika kilimo,”amesema Mhagama.
Amesema kilimohai kitafanya mazao ya wakulima yanunulike sana nchi za nje na kushauri ifanywe juhudi kilimohai kienee nchini.
Sixtus Ngonyani, akizungumza kwa simu kutoka Peramiho amesema amefurahi kusikia Tanzania sasa inatengeneza kiwanda cha mbolea isiyo na kimikali.
Siku hizo tulikuwa na mashamba darasa. Kila afisa lazima awe na shamba lake kila kijiji. Tuliwafundisha watu namna kutengeneza na kutumia vizuri mbolea.
Tulifanikiwa sana wakulima lazima wahimizwe kutumia mbolea, lakini pia wafundishwe kulinda afya ya udongo,”amesema Ngonyani.
Mkulima wa parachichi Mkoani Njombe, Erasto Ngole amesema alianza kutumia mbolea ya Hakika tangu ikiwa katika hatua ya majaribio na kwamba kwa kutumia mbolea hiyo anavuna kutoka kwenye mti mmoja wenye afya matunda makubwa na kupata sh. milioni 1.2 .
Mkulima wa Wilaya ya Wangingombe, Esther Msigwa amesema anafarijika kuona anapata mazao mengi kwa sababu ya kutumia mbolea ya kisasa. Nina shamba ekari moja na wamenifundisha namna nzuri ya kutumia mbolea hii. Matokeo ni mazuri,” ameeleza.
Wakala wa Pembejeo za kilimo wa Rungwe, Mkoani Mbeya, Daniel Mwakipesile amesema wakulima wanaelekea kuipenda mbolea ya hakika na kwamba ataendelea kuwa msambazaji wa mbolea hiyo.
Uzinduzi wa mbolea hii umenipa nguvu na hali ya kuendelea kuisambaza,amesema Mwakipesile
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbolea hiyo hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Guavay ambao ndilyo wazalishaji wa mbolea hiyo, Mhandisi Ahad Katera, alisema wamejipanga kuongeza uzalishaji kutoka tani 3,500 mpaka kufikia tani 20,000 kwa mwaka ili kukidhi mahitaji kwa wakulima.
Mkakati uliopo ni kuongeza uwezo wa kiwanda katika uzalishaji kwa kuongeza ajira 200 na mashine ili kupunguza uagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi, amesema Mhandisi Katare
Utafiti wa mbolea hiyo ulianza mwaka 2014 na kukamilika mwaka 2017 na ulishirikisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, Chuo cha Kilimo Cha Sokoine, Chuo Kikuu Cha Makerere, Tume ya Sayansi na Teknolojia na wadau wengine kupitia ufadhili wa Shirika la Bolnnnovate Afrika lenye makao makuu yake, Nairobi Kenya.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika