April 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi Mahomanyika wamlilia Rais Samia kuingilia kati mgogoro wa ardhi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAKAZI wa Mtaa wa Mahomanyika kata ya Nzuguni Jijini Dodoma wamemuomba Rais Samia kuingilia kati mgogoro wa ardhi kati ya wakazi hao na Jiji kwa kitendo wanachodai Jiji wanataka kuwapora maeneo yao.

Wakizungumza na vyombo vya habari jijini hapa Februari 25,2025 kwa nyakati tofauti Wananchi hao katika eneo la mgogoro siku ambayo walidai kuwaona maafisa wa jiji wakitaka kupima eneo hilo bila kuwashirikisha,wamesema kumekuwepo na  mgogoro wa miaka mingi wa kutaka kuporwa ardhi yao bila kupewa maelezo yoyote au uelezwa eneo hilo wanatakiwa kulipisha kwa matumizi gani na wanatakiwa wakazi hao kwenda wapi.

Mzee Daniel Mnyolwa (86) mmoja wa mwananchi anayedai kumiliki sehemu ya eneo hilo amesema kuwa  anasikitishwa na kitendo cha uongozi wa Jiji kwa kitendo cha kuwatuma wapimaji kwenda kupima ardhi hiyo bila kuwashirikisha wananchi wa eneo husika.

Akielezea kuwepo kwa wananchi katika eneo hilo Mzee Daniel amesema kuwa eneo hilo ni la asili na wamezaliwa na kulikuta na kuliendeleza hadi ambapo nao wana watoto,wajukuu na vitukuu.

“Mimi ni mzee kwa sasa nina miaka 86 nimezaliwa katika eneo hilo wakati huo vikiwa vijiji,tumekua na kuoa na kupata watoto,wajukuu na vitukuu alafu tunaambiwa hapa tumevamia.

“Tunajua kuwa ardhi ni ya serikali na serikali ni sisi inakuwaje tunajiwa na polisi wakiwa na mabunduki kwani sisi tupo wapi Kongo au Tanzania na je Serikali ni nani kama siyo sisi kwa hili tunaomba Rais Samia tusaidie kwa maana hapa kuna mchezo na Mungu anaona kilio chetu”ameeleza Mzee Daniel.

Naye Jane Bwanakoo mkazi wa eneo hilo amesema kuwa anaomba Rais Samia kuingilia mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi kwa kuwa wanaoathirika zaidi ni akina mama na watoto.

Amesema kuwa mgogoro huo ambao kwa sasa unazidi kukua na kuwafanya wananchi kukosa amani na kuna uwezo wa kutokea uvunjifu wa amani jambo ambalo halipendezi.

“Sisi hatuna shida na upimaji shida yetu ni kwani hatushirikishwi na kwanini tunapohoji tunapigwa na kukamatwa na hatufunguliwi kesi,mimi ni kati ya watu ambao nimeshapigwa na kuwekwa ndani lakini baada ya kuachiwa sikueleza kosa langu wala kupelekwa mahakamani kutoka na na hali hiyo inatusukuma kumuomba Rais kuona namna ya kutusaidia kama anavyosaidia watu wengine”ameeleza Jane.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahomanyika Abraham Aizaki amesema kuwa kilio cha wananchi wake ni kuona wanapewa maeneo yao kwa usalama bila kuwepo kwa Mtutu wa Bunduki.

Kiongozi huyo amesema tatizo hilo ni la muda mrefu na limekosa ufumbuzi kwani ni kama linahusisha pande tatu ambazo ni Jeshi,Jiji na wanachi jambo ambalo linasababisha sintofahamu.

Hata hivyo amesema kuwa kinachowachanganya wananchi hadi kufikia hatua ya kupaza sauti na kumpigia magoti kwa Rais ni  ili asikie kilio chao ni kutokana na suala la Jiji kutaka kupima maeneo hayo bila kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika wakati wameishi muda mrefu na eneo hilo lina hadi makaburi ya ndugu zao ya zamani.

“Rais ni kiongozi wa wananchi wetu sisi wote na anaongoza maskini na matajiri wanyonge na wenye furaha na ni sisi watu wa Chama cha Mapinduzi hivyo tunaomba asikie kilio chetu na atusaidie kama anasaidia wakazi wa maeneo mengine sisi hatutaki migogoro ila tunahitaji haki”ameeleza Mwenyekiti.

Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo lenye mgogoro siku inayofuata Februari 26,2025 Wananchi hao walifunga safari hadi zilipo Ofisi za  Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma ili kuomba waingilie kati suala hilo la  kuporwa ardhi, wakidai wanashinikizwa kuondoka kwenye maeneo yao kwa madai ya kuvamia sehemu tengefu la serikali.

Wakizungumza na waandishi wa habari,walivyofika katika Ofisi za Chama hicho wakazi hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mtaa, Abrahamu, wamesema wanaishangaa hali hiyo na kimya cha viongozi. 

“Tumeishi hapa kwa zaidi ya miaka 50, sasa tunashinikizwa na Jiji la Dodoma kwa kuwa tumeambiwa ni wavamizi wa maeneo yaliyotengwa,”amesisitiza Mputu.

Sarah Bwanakoo, mmoja wa wakazi hao, aliongeza kuwa ikiwa haki yao haitatolewa, watamtembelea Rais Samia Suluhu Hassan,Ikulu ili kutatua tatizo hilo.

 “Tumekuja hapa Ofisi za CCM Mkoa kumueleza Mwenyekiti, Alhaj Omary Kimbisa, kuhusu malalamiko yetu. Lengo letu si kufanya fujo tunataka msaada,” ameeleza.

Wakazi hao waliweza kufika katika ofisi za CCM Mkoa lakini walikosa kumwona Kimbisa na badala yake walizungumza na Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Charles Mamba, ambaye aliahidi kutembelea katika eneo hilo.

Hata hivyo siku chache baada ya malalamiko ya wananchi hao waandishi wa habari walifanya jitihada za kumtafuta   Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt.Frederick Sagamiko kwa njia ya simu ili aweze kulitolea ufafanuzi jambo hilo,alisema kuwa hayupo ofisini bali atafutwe siku ya jumatatu ambayo ni Machi 3, 2025.

Waandishi wa habari walivyomtafuta Ofisini kwake siku hiyo aliyoahidi atakuwepo,hakuwepo Ofisini kwake waandishi wa habari walielezwa kuwa hayupo ofisini yupo kwenye Kikao kazi cha Waziri na Wakuu wa Taasisi za Umma na Ofisi ameikaimisha kwa Kimaro na alipotafutwa kwa njia ya simu Dickson Kimaro alisema kuwa yupo nje ya ofisini naye amemkaimisha Afisa habari wa Jiji ambaye ni Denis Gondwe.

Naye Gondwe alipotafutwa Ofisi kwake hakuwepo na alipopigiwa simu alisema ana wageni mpaka hatakapomalizana nao hata hivyo hakueleza walikuwa wageni wa serikali au binafsi na atamalizana nao saa ngapi.