Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Rachel Kasanda amewataka wakazi wa Wilaya hiyo kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi wanapowakamata wahalifu.
Wakazi hao wametakiwa washirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama kwaajili ya kuwachukulia hatua za kisheria wahalifu wanaokamatwa.
DC Kassanda ametoa agizo hilo jana Jumatano Agosti 16, mwaka huu alipokuwa akizumgumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Bujashi kwenye ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo Wilayani humo pamoja na kuzungumza na kusikiliza kero za wananchi.
Akizungumza na Wananchi wa Bujashi, DC Kasanda amewaasa wakazi wa Kata hiyo kuacha tabia hiyo kwani ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi, kwasasabu vyombo vya ulinzi na usalama vipo kwaajili ya kutatua changamoto.
Amesema, wananchi wanapokamata mhalifu wanatakiwa kutoa taarifa katika mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Aidha, amewataka wakazi wa Magu kulinda na kuthamini miradi ya maendeleo iliyopo Wilayani humo ili iendelee kunufaisha wananchi na kuunga mkono juhudi za serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, DC Kasanda amewataka wazazi kuendelea kusimamia suala la maadili ya watoto haswa kukemea tabia ya utoro shuleni kwa watoto .
Kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hao, Dc Kasanda amewataka wananchi kuziwasilisha kwa viongozi wao kuanzia ngazi ya Kata ili uongozi wa Wilaya uzifanyie kazi.
DC Kasanda anaendelea na ziara ya kukagua shughuli za miradi ya maendeleo ambapo anatarajia kutembelea kata 25 za Wilaya ya Magu kuanzia Agosti 16 hadi 25 mwaka huu.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi