Na Chedaiwe Msuya, WF, Kigoma
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, Kanali Isaack Mwakisu amewataka Wananchi kukopa kwenye taasisi za fedha zilizosajiliwa na Serikali na kutambulika kwa kuwa itasaidia kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwa mkopaji kwa kuwa taasisi hizo zinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria.
Kanali Mwakisu alitoa rai hiyo baada ya kukutana na wataalam wa Wizara ya Fedha, TAMISEMI, Benki Kuu na wataalam wengine kutoka Taasisi za Serikali waliofika Wilayani mwake kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali.
Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa wananchi wanatakiwa kwenda kukopa Fedha kwenye benki na Taasisi nyingine za fedha zilizosajiliwa na zinazotambulika kisheria na siyo kwenda kukopa Fedha kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa na serikali,maarufu kama “kausha damu”.
“Matumizi ya Fedha ni muhimu sana, hivyo wananchi wasikope tu kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa,”amesisitiza Kanali Mwakisu
Aidha, Kanali Mwakisu amesema kuwa Serikali imekusudia kuhakikisha wananchi wengi wanapata uelewa wa masuala ya fedha ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika huduma rasmi za fedha.
“Wakulima msifanye matumizi mabaya ya Fedha zenu mnapo vuna mazao yenu bali fedha hizo zitumieni Kwenye matumizi sahihi ikiwemo kupeleka watoto shule,”ameongeza Kanali Mwakisu.
Kwa upande wake Stanley Kibakaya ambaye ni Afisa Usimamizi wa Fedha, Wizara ya Fedha, aliwataka wananchi wanapokopa waangalie viwango vya riba ndipo wakope na wanapokopa wahakikishe wanabaki na nakala ya mkataba ili panapotokea changamoto mkataba huo uwalimde.
Naye Abonaventula Frederick, mkaazi wa Kasulu aliishukuru Wizara ya Fedha kwa Kutoa Elimu hiyo ambapo aliiomba Serikali kuendelea kutoa Elimu katika maeneo mengine kwani asilimia kubwa ya wananchi hawajui wapi wanatakiwa kuhifadhi fedha zao na wapi wanatakiwa wakope.
“Wananchi wengi hawajui wapi pakuhifadhi fedha zao na wengi wamekopa sehemu ambazo siyo sahihi hali ambayo imesababisha wauze mali zao ikiwemo mashamba ili walipe mikopo wanayodaiwa, hivyo wengi wakipata elimu hii wataelimika,”amesema Frederick.
Aidha Stephanie Fulmasi amesema kuwa wamepata elimu kupitia filamu ambayo imeandaliwa na Wizara hiyo na kupitia filamu hiyo wamejifunza namna gani wakina mama wanatakiwa kwenda kukopa sehemu sahihi na siyo kukopa sehemu yenye riba kubwa.
Mafunzo ya elimu ya fedha yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Fedha yanalengo la kufikisha elimu na uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha.Kata zilizofikiwa mpaka sasa ni Buhingwe, Mnanila, Kinazi, Kasulu, Makere – VETA na Mvugwe.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato