November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi Kaliua wamshukuru Rais Samia kumaliza migogoro ya hifadhi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kaliua

WAKAZI wa Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora waliokuwa wanaishi katika vijiji vilivyokuwa ndani ya maeneo ya hifadhi wamemshukuru Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio chao na kuridhia vijiji hivyo visiondolewe.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea vijiji hivyo ili kujionea hali ilivyo sasa baada ya kurekebishiwa mipaka na kutambuliwa rasmi kisheria kuwa haviko ndani ya hifadhi wamesema wanajisikia faraja sana kwa uamuzi huo.

Mzee Jumanne Masanja (75) msukuma, mkulima, mkazi wa Kijiji cha Kasega, Kata ya Seleli ameishukuru serikali kwa kuwaruhusu kuishi katika eneo hilo kwani walifika hapo wakiwa vijana wadogo na sasa ni wazee, hawana nguvu tena.

Amebainisha kuwa kwa kipindi chote walichoishi katika eneo hilo walikuwa hawana amani kutokana na usumbufu, vitisho, vipigo, kunyang’anywa mifugo, kuchomewa nyumba na mazao na mengine mengi waliyokuwa wakifanyiwa.

‘Tunamshukuru sana Mhesh. Rais kwa kufanya maamuzi ya busara, tulikuja hapa tukiwa wadogo na tumeshakuwa wazee, hatuna sehemu ya kwenda tena, hata mazao tunayolima hayataharibiwa tena na Wahifadhi Misitu’, ameeleza.

Mkazi wa Kijiji cha Bulela katika kata hiyo, Ngomola Magembe (50) amesema kuwa sasa wanaishi vizuri, hawasumbuliwi tena na Maafisa Uhifadhi Misitu kama ilivyokuwa huko nyuma, wanalima na kufuga pasipo bugudha yoyote.

Sofia Kapezina, mkazi wa Kijiji cha Sasu katika Kata ya Sasu ameeleza kuwa Rais Samia ni Kiongozi mwenye maono mapana, uamuzi wake wa kumega maeneo ya hifadhi na kuongeza mipaka ya vijiji unaonesha jinsi anavyojali wananchi wake.

‘Mama ametuheshimisha sana, tuliteswa na kufukuzwa kama wanyama, tulichomewa nyumba, mazao na mifugo kuchukuliwa, lakini Mungu mkubwa, kamleta Rais anayetambua thamani ya wananchi wake, tunaomba Mwenyezi Mungu amlinde na amwepushe na balaa zote’, alisema.

Kaimu Mhifadhi Misitu wa Wilaya hiyo Sadock Gobanya amesema kuwa serikali imemaliza migogoro iliyokuwepo baina ya wananchi na Wakala wa Misitu baada ya kuainisha jumla ya Vijiji 22 vilivyokuwa katika hifadhi ya Mto Igombe wilayani humo na kuvitambua rasmi kisheria.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa zoezi hilo kumewezesha wananchi kuishi kwa amani katika vijiji hivyo na kumepunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya uvamizi wa maeneo ya hifadhi na kuimarisha usalama wa wananchi na ustawi wao.

Amebainisha kuwa utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni moja ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya CCM kama ilivyoelekeza katika ibara ya 73 (g) ya ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

Ametaja Vijiji vilivyoainishwa na kuwekewa vigingi (beacons) za mipaka mipya ili kutambuliwa rasmi kisheria kuwa ni Iyombo, Kagera, Kashishi, Busondi, Seleli, Mwendakulima/Katala, Nyasa, Bulela, Sasu, Mpagasha/Mhagasha, King’wangoko (Konanne), Ilege, Mkiligi, Nhwande, Mwongozo na Ibambo.

Vingine ni Mwanduti, Ntwigu, Imagi, Busanda, Ibapa na Kabanga ambavyo baada ya kufanyiwa tathmini vilionekana kuwa na sifa ya kuendelea kuwa na hadhi ya vijiji kama ilivyopendekezwa na kuridhiwa na timu ya wataalamu na Kamati ya Mawaziri 8 wa kisekta.

Afisa Misitu wa halmashauri ya wilaya hiyo Mussa Victor amefafanua kuwa migogoro ya matumizi ya ardhi ilileta uhasama mkubwa baina ya wananchi na serikali hivyo uamuzi huo umekuja wakati mwafaka na utachochea kasi ya maendeleo ya wilaya hiyo.

Kaimu Mhifadhi Misitu wa wilaya ya Kaliua Sadock Gobanya akionesha waandishi wa habari mipaka mipya iliyowekwa na serikali kwenye vijiji vilivyokuwa kwenye hifadhi za misitu.
Wakazi wa Kijiji cha Bulela wilayani Kaliua wakishiriki zoezi la uwekaji vigingi vya mipaka mipya hivi karibuni.