December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakandarasi wazalendo watakiwa kuzingatia mikataba

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WAKANDARASI wazalendo wameaswa kufanya kazi kwa weledi, ujuzi na maarifa ili miradi iwe bora kwa mujibu wa matakwa ya kimkataba wanayoingia kwa kuwa wazalendo na waadilifu na kuzingatia thamani ya fedha (value for money) kwa miradi mbalimbali wanayotekeleza.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Julai 13 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule,akitoa hotuba ya ufunguzi wa semina ya Wakandarasi wazalendo Tanzania iliyoandaliwa na Benki ya Diamond Trust Bank (DTB) kwa lengo la kuleta ushirikianonwa kibiashara kati ya Wakandarasi na Benki hiyo kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,Prof.Makame Mbarawa ambaye alitakiwa kuwa mgeni rasmi katika semina hiyo.

Senyamule amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amedhamiria kuboresha miundombinu katika Nyanja tofauti ikiwa ni pamoja na upanuzi wa Barabara, Ujenzi wa Barabara mpya kwa kiwango cha lami,Ujenzi wa reli ya mwendo kasi,Ujenzi wa kiwanja kipya cha kimataifa cha Ndege katika Jiji la DODOMA eneo la Msalato,Upanuzi na Ujenzi viwanja mbalimbali vya ndege hapa nchini,Ujenzi wa hospitali,Ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu na Miundombinu ya nishati ya umeme.

“Hivyo Wakandarasi na Watalaam washauri ni wadau muhimu sana katika tasnia ya ujenzi. Kupitia kandarasi mnazofanya, mnaijenga miundombinu ya nchi katika sekta mbalimbali. Manufaa ya moja kwa moja yanayopatikana kupitia ninyi ni pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi mmoja mmoja na hivyo kukuja kipato,

“Majukumu ya Mabenki ni kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara, makandarasi na wadau wengine hivyo nitoe rai kwenu kutumia fursa kikamilifu za kuongeza mitaji yenu kupitia benki ya Diamond (DTB) ili muweze kutekeleza kazi kandarasi zenu kwa ubora na wakati uliokusudiwa,pia ninawaasa kufanya marejesho ya mikopo kwa wakati ili Benki iweze kuboresha utendaji kazi wake na kupanua wigo zaidi kwa wadau wengine,”amesema Senyamule

Hivyo amesema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na wadau wake hususani mabenki na makandarasi na kuendelea kusimamia sera na miongozo mbalimbali pamoja na kuweka mazingira rafiki ili utendaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali iweze kuwa na ufanisi mzuri kwa ustawi uchumi wa nchi na wananchi wake.

“Sote tumehudhuria hapa katika kushiriki katika mafunzo haya mahususi kwa wakandarasi ili kupata uelewa zaidi juu ya masuala ya fursa za kifedha na Bima zitolewazo na Diamond Trust Bank.

“Ninatoa rai mliohudhuria semina hii mzingatie yale yatayoelezwa na waandaaji na mfanye majadiliano yenye tija ili kuimarisha sekta hii adhim ya Ukandarasi, Nimatumaini yangu kwamba kupitia semina hii fursa zaidi zitafunguka na hatimae kuweza kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za kifedha na bima ambazo wakandarasi wengi wamekuwa wakizipitia kwa muda mrefu,”amesema Senyamule.

Awali akitoa salam katika semina hiyo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Jabir Shekimweri amewataka wakandarasi hao kumshirikisha katika changamoto wanazopitia ili ikiwemo suala la kuchelewa kwa malipo ya miradi (certificate) kwani yeye hawezi kufahamu kama hajajulishwa.

“Niwaombe muwe mnanishirikisha ili tusaidiane kutatua changamoto hizi kwasababu Mkandarasi yupo kwenye Wilaya yangu halafu analalamika malipo wakati ninawezo wa kwenda kwa wakubwa na viongozi husika na jambo likatatuliwa hivyo naomba tuwe tunashirikiana mnapopata changamoto,”amesema Shekimweri.

Kwa upande wake Meneja wa Tawi wa DTB Mkoa wa Dodoma,Celsius Kizitto amesema kuwa semina hiyo imeshirikisha na wadau wengine kutoka Reliance Insurance na Jubilee Life ikiwa na lengo la kuweka mazingira mazuri ya kazi za ujenzi na wakandarasi.

Amesema kuwa lengo kubwa la semina hiyo ni kuhakikisha kwamba wakandarasi wazalendo wanapata huduma za kibenki pamoja na bima kwa wakati na gharama shindani.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha miundombinu kwenye upanuzi wa Barabara,ujenzi wa barabara mpya kwa kiwango cha lami,reli ya mwendo kasi,kiwanja cha ndege na madarasa vyote hivi vinamgusa moja kwa moja makandarasi ambaye ndiye mtekelezaji wa malengo haya ya mama yetu,

“Hili limetusukuma sisi kuona ni kwa namna gani tunaweza kumuunga mkono mama kwa kuwawekea mazingira rafiki wakandarasi kwenye upande wa benki na bima,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa Wakandarasi Taifa,Thobias Kyando akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wote ameiomba serikali kuona namna ya kuwashirikisha wakandarasi wazalendo kwenye miradi mikubwa na wakandarasi wa kigeni ili wawe na uzoefu na ujuzi kwa kinachofanyika ila wanapomaliza miradi na kuondoka serikali isipate gharama ya kuwaita tena pindi miradi inapohitaji matengenezo.

“Kwa mfano sasa hivi wanajenga uwanja wa ndege wakimaliza wakondoka tusipokuwa na ujuzi nani atafanya maintenance kama siyo serikali kuingia tena gharama ya kuwaita tena,”amesema Kyando.

Pia amesema kuwa wao kama wakandarasi wamekuwa na changamoto ya kucheleweshewa malipo hadi mwaka kitendo kinachowafanya wasiaminiwe na mabenki pamoja na wasambazaji wa vifaa kwa kuchelewa kuwalipa.