October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akicheza mziki uliokuwa ukipigwa na Msanii Hamza Kalala na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally Kakurwa katika hafla hiyo ya Chakula cha Mchana kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Wajumbe Mkutano Mkuu CCM, wageni wajionea maajabu Ikulu Chamwino

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Chamwino

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na wageni mbalimbali zaidi ya 6,500 leo wametembelea Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya kujionea mambo makubwa yaliyofanywa na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Rais John Magufuli.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na Rais Magufuli kwa wajumbe hao,Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa amesema wajumbe waliotarajiwa walikuwa 4,000, lakini kwa mapenzi mema wageni wageni wameongezeka zaidi ya 2,000.

Msigwa amesema wajumbe hao wamepitishwa katika majengo ya Ikulu, likiwemo jengo lililojengwa na Mwenyekiti wa Kwanza na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baba wa Taifa Marehemu Julius Nyerere mwaka 1969 na lililojengwa mwaka 1973 na kujionea majengo yote ambayo Rais Magufuli ameongeza ikiwemo ujenzi wa ukuta.

Msigwa amesema Rais Magufuli amepanua wigo wa eneo la Ikulu kutoka hekari 61 hadi kufikia hekari 8,473 na kulifanya eneo hilo kuwa kubwa kuliko maeneo ya Ikulu zote Duniani.

“Dkt. Magufuli amepanua ukubwa eneo hilo,lakini pia amejenga barabara za ndani na ujenzi wa Ikulu umekamilika.” Amesema Msigwa.

Pia amewaeleza wajumbe kuwa katika eneo hilo la Ikulu limetengenezwa eneo la kivutio (utalii) ambapo kuna wanyama na wageni mbalimbali wanaotembelea Ikulu watapata fursa ya kutembelea eneo hilo la utalii la Ikulu ambalo lina wanyama wa aina mbalimbali takriba 5,000.

Aidha amesema jumla ya kilometa 68.8 za barabara zimejengwa ili kuwafikia wanyama hao .

Kwa mujibu wa Msigwa katika eneo hilo yamejengwa mabwawa nane yenye baridi pia kuna vilima ambavyo huufanya mji wa Dodoma kuonekana vizuri.