Na Yusuph Mussa,TimesMajira Online. Korogwe
BAADHI ya wajasiriamali wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, wamesema wana imani na Rais Dkt. John Magufuli kuwa atamaliza changamoto zao za kupata mitaji kwa kupewa mikopo nafuu kutoka halmashauri, hasa baada ya mitaji yao kufa kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona.
Wakizungumza mjini hapa jana mara baada ya Dkt. Magufuli, kuapishwa kipindi cha pili kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, wajasiriamali hao wamesema kuingia kwa ugonjwa wa Corona nchini Machi 16 na Machi 17 mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza kufunga shughuli zenye mikusanyiko mingi, biashara zao mbalimbali ziliyumba.
Mjasiriamali Joyce Semgaya, ambaye anashona nguo katikati ya Soko Kuu la Manundu mjini Korogwe amesema, wameshindwa kukopa mikopo kwenye sekta binafsi sababu mikopo hiyo ina riba kubwa, lakini anaamini mikopo ya halmashauri ambapo wanawake wana asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili itawapa nafuu.
“Tuna imani na Rais Magufuli katika kushughulikia kero za wananchi. Sisi ni wajasiriamali, lakini wakati wa Corona mitaji yetu ilikata. Na hata sasa bado hatujarudi kwenye hali yetu ya kawaida.
“Hivyo tunaomba mikopo inayotolewa na halmashauri itufikie na sisi wananchi wanyonge. Mimi na wenzangu tumewahi kuomba mkopo, lakini hatukupata. Lakini kwa miaka mingine hii mitano, tunaweza kupata mikopo hiyo,” amesema Semgaya.
Mariam Mussa ambaye anamiliki Mgahawa wa Embassy uliopo Soko Kuu la Manundu mjini Korogwe amesema biashara yake iliyumba kwa zaidi ya miezi sita kutokana na ugonjwa wa corona, lakini anaamini mikopo inayotolewa na halmashauri safari hii itamfikia.
“Nimekuwa nafanya biashara hii ya mamalishe tangu mwaka 1982 kwenye soko hili la Manundu, lakini sijawahi kupata mikopo. Na huwa tunahamasishwa sana kujiunga na vikundi vya ujasiriamali, lakini bado hatupati.
“Nina imani baada ya Rais Magufuli kuapishwa ili kumalizia kipindi chake cha pili, watapata mikopo hiyo. Na hiyo itatuongezea mitaji yetu ambayo ilitetereka kutokana na corona” amesema Mussa.
Naye Abdulrahman Uledi ambaye ni fundi wa kushona nguo Soko Kuu la Manundu, amesema ni matumaini yake kuwa Rais Magufuli ataendelea kuibadilisha Tanzania kwa kuijengea miundombinu ya barabara. Lakini pia ataboresha kipato cha mtu mmoja mmoja hasa kwa vijana wanaojishughulisha na kazi mbalimbali za ujasiriamali.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Manundu Kati, Mussa Hussein amesema ni kweli kuna kilio kikubwa cha baadhi ya wajasiriamali kutaka nao wapate mikopo. Na baadhi ya maombi ya wajasiriamali, wameshawasilisha Ofisi ya Halmashauri, lakini anaamini Serikali ya awamu ya tano itaendelea kutoa mikopo zaidi kwa wajasiriamali kupitia ile asilimia 10 ya mikopo kwa wanawake, vijana na walemavu.
Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mbeza Neema Shemu ambako ndipo lilipo Soko Kuu la Manundu, amesema kuna baadhi ya vikundi vya vijana wauza samaki Soko Kuu la Manundu pamoja na wanawake wa soko hilo waliomba mikopo, lakini hajapata mrejesho kama walipata.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Korogwe Charity Sichona amesema kuna vikundi vimepata mikopo kwenye halmashauri hiyo ikiwemo vijana wauza samaki wakavu wa Soko Kuu la Manundu mjini Korogwe ambao wamepata sh. milioni sita mwaka jana, lakini changamoto iliyopo ni kuwa baadhi ya vikundi havirejeshi fedha hizo ili wengine wakopeshwe.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â