Na Suleiman Abeid, Shinyanga
WAUMINI wa Kiislamu mjini Shinyanga wameendelea kumpongeza na kumshukuru Rais John Magufuli kwa msimamo wake thabiti wa kutozifunga nyumba za ibada kwa hofu ya ugonjwa wa COVID – 19.
Pongezi hizo zimetolewa jana na waumini wa kiislamu wa msikiti wa Mufti Issa Shabani Simba uliopo mjini Shinyanga. Wamesema Rais Magufuli ameonesha imani yake ya dhati kwa Mwenyezi Mungu kutokana na muda wote kuwaomba Watanzania wamtegemee na kumuomba zaidi Mungu ili awaepushe na ugonjwa huo.
Wamesema msimamo wake umekuwa tofauti na baadhi ya viongozi wenzake katika mataifa mengine duniani ambao kutokana na hofu ya ugonjwa wa COVID – 19 waliamua kufunga nyumba za ibada na kuzuia wananchi wao kutotoka ndani kwa vipindi virefu.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu kwa msimamo wake wa kutoteteleshwa na ugonjwa wa COVID -19 na badala yake kuwataka watanzania wasimame katika maombi muda wote kumuomba mwenyezi mungu atuondoshee gonjwa hili,”amesema.
“Yeye badala ya kuwazuia Watanzania kutokutoka ndani au kufunga nyumba za ibada aliruhusu tuendelee na shughuli zetu za kila siku akisisitiza suala la kuchukua tahadhari wakati wote kwa kunawa mikono yetu kwa maji tiririka na kuvaa barokoa pale penye mikusanyiko ya watu wengi,” alieleza Abdalah Kilobi.
Kilobi msimamo wa Rais Magufuli tayari umeanza kuigwa na mataifa mengine likiwemo taifa kubwa la Marekani ambako Rais Donald Trump juzi amesikika akiamuru nyumba zote za ibada nchini humo zifunguliwe na pia wananchi waondolewe vizuizi na badala yake waendelee kufanya shughuli zao uamuzi ambao Rais Magufuli alikuwa nao tangu awali.
Kwa upande wake Sheikh wa Kata ya Mufti Issa Shabani Simba, mjini Shinyanga Barulisa aliwataka waumini wa kiislamu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuumaliza kwa amani na salama mwezi mtukufu wa Ramadhani na pia kumpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa jinsi alivyowahimiza Watanzania wazidishe maombi kwa mwenyezi mungu ili auondoe ugonjwa wa COVID – 19.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kumaliza salama mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, lakini pia tunampongeza na kumshukuru Rais wetu, Dkt. Mafuguli kwa kusimama na watanzania katika maombi muda wote kumuomba Mwenyezi mungu atuepushe na janga hili,”
“Rais wetu amekuwa na msimamo tofauti na viongozi wengi katika mataifa mengine, ambapo kaonesha mfano wa pekee wa kutobabaika kutokana na ugonjwa huu, na badala yake muda wote amekuwa akituhimiza tuzidishe maombi kwa mwenyezi mungu ili atuepushe na gonjwa hili, na kuzuia nyumba za ibada zisifungwe,” alieleza Sheikh Barulisa.
Sheikh huyo amesema kuna kila sababu ya kila Mtanzania kumuombea maisha mema Rais Dkt. Magufuli ili aendelee kuongoza nchi kwa amani na salama na kwamba mwenyezi mungu amuonesha njia iliyo sahihi katika uongozi wake na wao hawana cha kumlipa, bali Mungu ndiye anayejua malipo yake.
More Stories
Madiwani Ilala watoa chakula kwa watoto yatima
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano