November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waislam watakiwa kuchunga uadilifu nchi ipate kuongoka

Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraOnline,Zanzibar

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Alhaj Othman Masoud Othman, amewahimiza Waumini wa Kiislamu juu ya kutenda uadilifu kwani kufanya hivyo ndiko kunakopelekea kuongoka kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Othman ameyasema hayo leo katika nasaha zake mbele ya Waumini wa Kiislamu pale alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa, huko  Msikiti wa Miembeni Chake-Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema kuwa sifa ya uadilifu inajenga heshima, amani na kuaminiana miongoni mwa watu, hali ambayo inaitengeneza jamii ya watu ambao wanasongambele kimaendeleo na siyo kurudi nyuma.

“Tulipokosea ni hapo; na hiyo ndiyo sababu kubwa ya mambo kuharibika ndani ya jamii na katika Nchi yetu kwa ujumla”, ameongeza Mheshimiwa Othman akisisitiza juu ya tija ya kutenda uadilifu.

Aidha, akifafanua kuhusu hali halisi, na madhara ya kukusekana uadilifu, Mheshimiwa Othman amesema, “tunachoshuhudia sasa katika Nchi, ndugu zangu ni vurugu; fitna ya ndugu kwa ndugu, jirani kwa jirani, na hata raia mbele ya watawala”.

Hivyo ameeleza kwamba ili kufaulu ‘mitihani’ pamoja na kuyaongoza mambo kwa mafanikio katika jamii, ni wajibu pia kuzingatia Mafunzo yote aliyokuja-nayo Mtume (S.A.W.) huku akisema, “naamini kwamba tukizingatia hayo utakuwa msingi wa kila mmoja wetu kuokoka na kupata nusra maishani na Mbele ya ALLAH (SW).

Akiongelea haja ya Mamlaka kuzingatia uadilifu wa watu kabla ya kuwapatia nafasi za kuongoza katika sekta mbalimbali Nchini, Mheshimiwa Othman amesema, “jambo la kushangaza hapa kwetu, anatafutwa yule anayeukataa uadilifu ndipo anapewa uongozi”.

Akitanguliza salamu zake kwa Waumini waliohudhuria Msikitini hapo, Mratib wa Ofisi ya Mufti kisiwani Pemba, Sheikh Said Mohamed amesema amani itaweza kuenea na kuendelea kwa maisha yote,  jamii na Nchini kote, pindipo watu watatekeleza kwa vitendo Mawaidha mema wanayopewa kila siku, yakiwemo ya kuzingatia uadilifu, na katika ngazi zote.

Akitoa Khutba Mbili wakati wa Ibada hiyo, Khatiib Sheikh Khalifah Mrisho, amesema nusra ya mwanadamu kupitia Mitihani ya Maisha, Duniani na baadae huko Akhera, itapatikana kwa kutekeleza kikamilifu Maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kufuata Mwenendo Mwema wa Kiongozi wa Umma wa Kiislamu, Mtume Muhammad (S.A.W.).

“Ndugu zangu Waislamu maisha yetu yote ni ya kujaribiwa, bali njia ya kufaulu ni kwamba sisi tunacho Kigezo Chema Mtume wetu (S.A.W.); Safari yetu ni ngumu, ina shida, na hasa tukiangalia namna ya Mauti na pale wakati wa Mmoja miongoni mwetu anapokata Roho, panahitaji mazingatio makubwa”, amesema Sheikh Khalifa.

Waumini wa Msikiti huo, wakiongozwa na Imam Sheikh Omar Ali Salim, wameeleza faraja kubwa waliyoipata kutokana na Ujio wa Mheshimiwa Othman Msikitini hapo wakisema, “hii imekuwa ni faraja ya Pemba nzima”.

Mamia ya Wananchi na Waumini wa Kiislamu, wamemlaki Mheshimiwa Othman alipowasili katika maeneo ya Msikiti huo, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Bw. Mattar Zahor Masoud; pamoja na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar,Salim Abdallah Bimani.