October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu kidato cha sita waitwa JKT

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limewaita vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita kwa mwaka 2024 kutoka shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2024 .

Akizungumza Mei 24 mwaka huu na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya JKT Chamwino mkoani Dodoma,Brigedia Jenerali Mabena amesema,tayari Jeshi hilo limewapangia makambi watakayo kwenda kupatiwa mafunzo.

Amesema,vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia Juni Mosi hadi Juni 7,mwaka huu .

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena , vijana hao wamepangwa katika Kambi za JKT Rwamkoma -Mara, JKT Msange – Tabora , JKT Ruvu – Pwani , JKT Mpwapwa , Makutupora JKT- Dodoma na JKT Mafinga – Iringa.

Makambi mengine waliyopangiwa ni JKT Mlale – Ruvuma , JKT Mgambo na JKT Maramba – Tanga , JKT Makuyuni – Arusha , JKT Bulombora , JKT Kanembwa na JKT Mtabila – Kigoma , JKT Itaka- Songwe , JKT Luwa na JKT Milundikwa – Rukwa , JKT Nachingweq – Lindi , JKT Kibiti – Pwani na Oljoro JKT- Arusha.

Aidha amewataka vijana hao kuripoti wakiwa na vifaa mbalimbali vikiwemo bukta ya rangi ya ‘Dark Blue’ yenye mpira kiunoni , iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini, isiyo na zipu, T- shirt ya rangi ya kijani , Raba za michezo rangi ya kijani/ blue, shuka mbili za kulalia zenye rangi ya blue bahari,soksi ndefu za rangi nyeusi na track suit ya rangi ya kijani/bluu,.

Vile vile amewataka kuripoti makambini wakiwa na nyaraka zote zinazohitajika katika udahili wa kujiunga na elimu ya juu , zikiwemo cheti cha kuzaliwa , vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na nauli ya kwenda makambini na kurudi nyumbani,”

Brigedia Jenerali Mabena amesema orodha kamili ya majina ya vijana hao , Makambi ya JKT waliyopangiwa na maeneo makambi hayo yalipo na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo , inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz