Na Severin Blasio,TimesMajira Online. Mvomero
WAHITIMU wa darasa la saba Shule ya Msingi Tangeni Wilaya ya Mvomero mkoani hapa, wametahadharishwa kuwa makini na maisha ya mtaani baada ya kumaliza elimu ya msingi, kwani kuna uharibifu mwingi kwa vijana wadogo hususan wasichana kupata mimba na hatimaye kutelekezwa.
Mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi, wasichana imebainika wamekuwa wakipata mimba na kuathiri ndoto ya kwenda sekondari huku wavulana, wakiharibikiwa kwa kujiingiza katika makundi yasiyofaa hata ya kutumia dawa za kulevya kama bangi.
Rai hiyo imetolewa na Padre Emil Kobero, aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo na kuwataka wazazi kuwaangalia kwa makini watoto wao wakati wakiwa nyumbani, baada ya mitihani yao ya darasa la saba.
Padre Kobero ambaye ni Paroko wa Parokia ya Tangeni Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo Morogoro na mshauri wa vijana Jimbo Katoliki Morogoro amesema, kuhitimu darasa la saba ni hatua ya kwenda sekondari hivyo baada ya mitihani yao watoto hao, wanapaswa kupumzika na kujiandaa kwenda sekondari na si kujiingiza katika makundi mabaya.
Amesema ushirikiano wa karibu baina ya wazazi, walezi na uongozi wa serikali, unahitajika katika kupambana na waharibifu wa watoto ambapo alisikitika kuona baadhi ya wazazi, wakifumbia macho uovu na ukatili unaotendwa kwa watoto wao kwa sababu ya rushwa wanayopewa na watu wanoharibu watoto hao.
Ametaka serikali, kuchukua hatua kali zinazopaswa kwa wazazi wanaoficha uovu ili kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi