November 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahasibu watakiwa kukabiliana na mabadiliko ya Teknolojia

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

MHASIBU Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, amewataka wahasibu kuzingatia maelekezo ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kuhusu namna ya kuripoti masuala ya mabadiliko ya tabianchi,teknolojia na kutumia fursa zilizopo ili kuboresha uzalishaji wa kiuchumi na kuchangia katika maendeleo endelevu Nchini.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika Mkutano mkuu wa mwaka 2024 wa bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Leonard Mkude ameeleza kuwa wahasibu wana nafasi muhimu katika mnyororo wa uzalishaji wa kiuchumi, hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia kama vile matumizi ya akili bandia katika ukuaji wa uchumi.

“Wahasibu ni kiungo muhimu katika mipango na matumizi ya fedha, hasa katika juhudi za Tanzania kufikia uzalishaji wa hewa chafu sifuri ndani ya miaka 50,” amesema CPA Mkude.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Prof. CPA Sylvia Temu, amesema Mkutano huo wa siku tatu una malengo mawili makuu, likiwemo kubadilishana maarifa na uzoefu wa kitaaluma ili kubaini fursa na changamoto zinazokabili tasnia ya uhasibu.

“Pia tumejadili uelekeo wa nchi kwa miaka 25 ijayo, ambapo wahasibu wanapaswa kushiriki kikamilifu kubaini fursa za kuendeleza uchumi wa taifa letu na kuleta mchango wenye thamani katika maendeleo ya nchi,” amesema Prof. Temu

Mwanachama wa heshima wa NBAA, CPA Saimon Sayore, amewataka vijana kuipenda taaluma ya uhasibu, kuitumikia kwa uaminifu, na kuhakikisha wanatunza vyema fedha za taasisi na taifa kwa ujumla.

Mkutano huo unajumuisha mawasilisho na majadiliano mbalimbali yanayolenga kutoa suluhisho kuhusu mchango wa wahasibu katika kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na kuimarisha maendeleo endelevu.