January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahamiaji haramu 158 wakamatwa Shinyanga ndani ya miezi mitatu

Na Suleiman Abeid,TimesMajira online,Shinyanga

IDARA ya Uhamiaji Mkoani Shinyanga imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 158 ndani ya kipindi cha miezi mitatu cha Januari hadi Machi, 2021 wakituhumiwa kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha Sheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Ofisa Uhamiaji wa mkoa, Rashidi Magetta kwa waandishi wa habari mkoani Shinyanga kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na operesheni za kushitukiza zinazofanyika mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga.

Amefafanua Magetta alisema miongoni mwa watuhumiwa hao wapo waliofikishwa mahakamani kulingana na uzito wa makosa yao wakiwemo raia 40 kutoka nchini Ethiopia na wale waliobainika kuishi na kuendesha maisha yao hapa nchini kinyume cha sheria walirejeshwa nchini kwao.

Hata hivyo amesema mtuhumiwa mmoja amefikishwa mahakamani ili kuweza kuthibitisha uraia wake baada ya kudai yeye ni Mtanzania wakati anahisiwa siyo raia na hivi sasa kesi yake namba CC.08/2021 inaendelea katika mahakama ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Amesema mbali ya kukamatwa kwa raia kutoka nchini Ethiopia wahamiaji wengine waliokamatwa wanatoka katika nchi za Burundi, Rwanda, Kenya, Mongolia, Indonesia, Pakistan, China na India ambapo watuhumiwa 57 walifikishwa mahakamani na kati yao 56 walihukumiwa kutumikia adhabu ya vifungo kati ya miezi miwili na mitatu.