Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
WAGOMBEA saba wa Ubunge katika Jimbo la Ilemela na mawakala wao kutoka vyama mbalimbali vya siasa wameapishwa kwa ajili ya kuingia kwenye vituo vya kuhesabia kura za Rais, Ubunge na udiwani kwa ngazi ya Kata katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuapisha wagombea hao, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela, John Wanga amesema, kati ya vyama vya siasa vilivyochukua fomu ya uteuzi ni saba tu vilivyokidhi masharti ya uteuzi huo.
“Vyama vilivyokidhi masharti ni CCM, ADC, ACT Wazalendo, CHADEMA, DP, Demokrasia Makini na NRA na leo hii wanaapishwa ili wapate fursa ya kuingia kwenye vituo vya majumuisho ya kura za Rais, Ubunge na Madiwani kwa ngazi ya Kata,” amesema Wanga.
Amesema, Jimbo hilo lina vituo vya kupigia kura 795, vilivyogawanyika katika Kata 19 kwa idadi tofauti vikiwa na wapiga kura 302,589 walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Pia amesema kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeleta vifaa mbalimbali vya uchaguzi katika Jimbo hilo ambapo mpaka sasa vilivyopokelewa vinafikia asilimia 90 ya vifaa vinavyohitajika na maandalizi yapo vizuri na uchaguzi utafanyika kwa ufanisi kadri ilivyopangwa.
Majumuisho ya kura za Urais na Ubunge yatafanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mara baada ya zoezi la ipigqji kura kukamilika.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wote wa Jimbo hilo waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura kujitokeza kwa wingi siku ya Jumatano Oktoba 28 mwaka huu kwani vituo vitafunguliwa kuanzia saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni.
Wanga pia ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wananchi, viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, madhehebu ya dini na watanzania wote wenye mapenzi mema kuitunza, kuilinda na kuienzi amani katika kipindi chote kabla ya siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi huku mawakala kutoruhusiwa kuingia na simu katika chumba cha kuhesabia na kujuishia kura.
Baada ya kuapishwa, Mgombea Ubunge Jimbo la Ilemela kupitia CCM DKt. Angeline Mabula amesema, msimu wa kampeni umeenda vizuri na mahudhurio ya watu yapo vizuri hivyo Oktoba 28 wananchi wajitokeze kwa wingi Katika kupiga kura.
“Kazi tumefanya na zinajidhihirisha,tumetekeleza sana kazi kwa kipindi kilichopita,wanailemela ni mashahidi kwa miaka kumi uliopita na mitano ya sasa Ilemela kuna mabadiliko makubwa,hivyo naomba watupatie tena ridhaa ya wananchi kuchagua Chama chetu,” amesema Dkt. Angeline.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba