Na Mwandishi wetu, timesmajira
WALIOKUWA Wagombea Udiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) katika Kata za Rugongwe, Mukabuye na Nyaruyoba kwenye uchaguzi Mkuu 2020 wamejiunga ACT Wazalendo na kupokelewa na Katibu Mkuu wa Chama Ado Shaibu.
Akitaja madiwani hao ni Godwin Sibanilo, aliyekuwa Diwani wa Chadema Kata ya Nyaruyoba (2015-2020) na Mgombea Udiwani mwaka 2020,Esrom Masunzu aliyekuwa Mgombea Udiwani Kata ya Rugongwe na Rogers Philemon, aliyekuwa Mgombea Udiwani Kata ya Mukabuye.
Akizungumza hayo jana kwenye Mkutano Mkuu wa Jimbo la Muhambwe uliofanyika juzi, Katibu Mkuu Ado Shaibu aliwakaribisha wanachama hao wapya kuendeleza mapambano ya kuwakomboa Wana Kibondo, Kigoma na Watanzania.
“Kwa hakika mmejiunga na Chama makini, Karibuni tuendeleze mapambano ya kuwakomboa Watanzania. Hakuna Chama kimefanya juhudi kubwa ya ujenzi wa Chama mkoani Kigoma baada ya Uchaguzi Mkuu 2020 zaidi ya ACT Wazalendo,”alisema na kuongeza
“Ndio maana, hata nikisikia wengine wana Operesheni hapa, sijawahi kukosa usingizi kama Katibu Mkuu wenu,najua Kigoma ni ngome yetu imara hivyo uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, tunalenga kuonesha nini maana ya “Kigoma ya Zambarau” kwa kushinda viti vingi zaidi,”amesisitiza
Mbali na waliokuwa wagombea udiwani, pia Katibu Ado Shaibu alimpokea Abubakari Kabamvu aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee (BAZECHA) Wilaya ya Kibondo, Elizabeth Matanywa, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) Kata ya Bitale na Justine Kapesa aliyekuwa Kiongozi wa Red Brigade.
Katibu Mkuu Ado Shaibu anaendelea na ziara ya kutembelea majimbo Mkoani Kigoma ambapo kwa kila Jimbo anakutana na viongozi wa Kata zote kupitia mikutano Mikuu ya Majimbo.
Ado ameshatembelea majimbo ya Kigoma Mjini, Kigoma Kaskazini, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini, Buyungu na Muhambwe. Leo atahudhuria Mkutano Mkuu wa Jimbo la Buhigwe. Ziara ya Katibu Mkuu Mkoani Kigoma itahitimishwa kesho ambapo anatarajiwa kushiriki Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kigoma Kusini.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua