January 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafugaji waomba elimu kuboresha shughuli zao

Na Allan Vicent,n TimesMajira Online, Uyui

WAFUGAJI zaidi ya 100 kutoka katika kata zote 30 za Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora wameomba kupatiwa elimu ya ufugaji bora na maeneo ya malisho ili kuboresha shughuli zao ikiwemo kuongeza idadi ya mifugo ila sio kupunguza.

Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji (CCWT) Wilayani humo Godfrey Michael ambapo alieleza kuwa wanachohitaji ni kupewa mbinu za ufugaji bora ili kuongeza uzalishaji wa mifugo na kitoweo cha nyama.

Alisema malengo yao yanaendana na dhamira ya serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo ameendelea kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanda vya nyama.

Alibainisha kuwa uhitaji wa kitoweo cha nyama na mazao mengine yatokanayo na mifugo bado ni mkubwa hivyo wanahitaji ni elimu zaidi itakayowasaidia kufuga kwa tija ili kuongeza mifugo na uzalishaji mazao yatokanayo na mifugo hiyo.  

Michael alifafanua kuwa migogoro baina ya wakulima na wafuagji imekuwa ikisababishwa na ukosefu wa maeneo rasmi ya malisho hivyo akasema kukamata mifugo yao na kuwapiga faini ya mamilioni ya fedha, hakuna tija kwa mfugaji.

Mwenyekiti Mstaafu wa Wafugaji Wilayani humo Seni Simon (75) aliomba uongozi wa halmashauri  kuwasaidia ili kila kata iwe na josho na kuongeza maabara za mifugo ili kuboresha zaidi mifugo yao.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo juzi kwenye mkutano wao katika ukumbi wa halmashauri Mkuu wa Wilaya hiyo Kisare Makori alisema Wilaya hiyo sasa ina jumla ya ng’ombe 441, 190, mbuzi 152, 180, kondoo 72,118 na kuku 911,372.

Alifafanua kuwa Wilaya hiyo ina jumla ya hekta 457, 400 sawa na km za mraba 11,806 na kubainisha kuwa eneo linaloweza kutumika kwa malisho ni jumla ya hekta 711, 884 hivyo eneo hilo kutotosheleza malisho ya mifugo iliyopo.

Alisisitiza kuwa idadi ya watu na mifugo imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa wakati eneo la ardhi lililopo likibakia vile vile, hivyo kutoruhusu ufugaji wa kuhama hama kama ilivyozoeleka kwa wafugaji walio wengi hususani wasukuma.

DC alieleza kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekusudia kuinua sekta hii ili iwanufaishe wafugaji na jamii nzima, hivyo akawataka kuanza kufuga kisasa ikiwemo kuwa na mifugo michache ili ilete tija kubwa katika maisha yao.

Alitaja baadhi ya faida za ufugaji huo kuwa ni kuepusha migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji, kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama, ngozi na kwato hivyo kujipatia fedha nyingi zitakazochochea mapato ya taifa,

Alibainisha changamoto za ufugaji holela wa kuhamahama kuwa ni uharibifu wa mazingira, miundombinu ya barabara na madaraja na kuongeza migogoro baina ya wakulima na wafugaji kwa kupitisha au kulisha mifugo hiyo katika mashamba yao.

Mamia ya wafugaji katika halmashauri ya Wilayaya Uyui Mkoani Tabora wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo juzi ambapo waliomba kupewa elimu ya ufugaji bora na malisho huku wakibainisha kuwa kupunguza mifugo ni umaskini .Picha na Allan Vicent