Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Uyui
WAFUGAJI Wilayani Uyui Mkoani Tabora wameomba kutengewa maeneo maalumu ya malisho na kujengewa majosho ya kutosha ili kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao yake kwa manufaa yao na taifa .
Akizungumza na gazeti hili juzi kwa niaba yao, Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji (CCWT) Wilayani hapa Godfrey Michael alisema ukosefu wa maeneo maalumu ya malisho na majosho ya kutosha ni kikwazo kikubwa kwa wafugaji hapa nchini.
Alibainisha kuwa licha ya dhamira njema ya serikali kuinua wafugaji lakini hakuna mkakati wote kwa Wizara husika kuanza kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji licha ya kuwepo maeneo mengi ya hifadhi na mapori ambayo hayatumiki kwa shughuli zozote.
Aliomba Kikosi cha Mawaziri 8 kilichopewa kazi maalumu ya kupitia maeneo yote ya hifadhi na mapori yenye migogoro na kuitafutia ufumbuzi kutumia fursa hiyo kubainisha maeneo yanayofaa kwa ajili ya shughuli za wafugaji.
Aliongeza kuwa kama watatengewa maeneo maalumu ya kufanyia shughuli zao watafanya ufugaji wenye tija na mifugo yao itakuwa na afya njema, watakachohitaji ni kuongezewa mbinu za ufugaji bora ili kuongeza uzalishaji.
Mwenyekiti alisisitiza kuwa malengo yao yanaendana na dhamira ya serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha uwekezaji katika sekta zote ikiwemo sekta ya mifugo, mfano ujenzi viwanda vya nyama.
Alibainisha kuwa uhitaji wa kitoweo cha nyama na mazao mengine yatokanayo na mifugo bado ni mkubwa ndani na nje ya nchi hivyo wanahitaji elimu pia itakayowasaidia kufuga kwa tija na kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo.
Michael alifafanua kuwa migogoro baina ya wakulima na wafuagji imekuwa ikisababishwa na ukosefu wa maeneo rasmi ya malisho hivyo akasema kukamata mifugo na kuipiga mnada au kuwapiga faini ya mamilioni ya fedha hakusaidii.
Mwenyekiti Mstaafu wa Wafugaji Wilayani humo Seni Simon (75) aliomba uongozi wa halmashauri kuwasaidia ili kila kata iwe na josho na kuongeza maabara za mifugo ili kuboresha zaidi mifugo yao.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo juzi kwenye mkutano wao katika ukumbi wa halmashauri Mkuu wa Wilaya hiyo Kisare Makori alisema Wilaya hiyo sasa ina jumla ya ng’ombe 441, 190, mbuzi 152, 180, kondoo 72,118 na kuku 911,372.
Alifafanua kuwa Wilaya hiyo ina jumla ya hekta 457, 400 sawa na km za mraba 11,806 na kubainisha kuwa eneo linaloweza kutumika kwa malisho ni jumla ya hekta 711, 884 hivyo eneo hilo kutotosheleza malisho ya mifugo iliyopo.
Alisisitiza kuwa idadi ya watu na mifugo imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa wakati eneo la ardhi lililopo likibakia vile vile, hivyo kutoruhusu ufugaji wa kuhama hama kama ilivyozoeleka kwa wafugaji walio wengi hususani wasukuma.
DC alieleza kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekusudia kuinua sekta hii ili iwanufaishe wafugaji na jamii nzima, hivyo akawataka kuanza kufuga kisasa ikiwemo kuwa na mifugo michache ili ilete tija kubwa katika maisha yao.Alitaja baadhi ya faida za ufugaji huo kuwa ni kuepusha migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji, kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama, ngozi na kwato hivyo kujipatia fedha nyingi zitakazochochea mapato ya taifa.
Alibainisha changamoto za ufugaji holela wa kuhamahama kuwa ni uharibifu wa mazingira, miundombinu ya barabara na madaraja na kuongeza migogoro baina ya wakulima na wafugaji kwa kupitisha au kulisha mifugo hiyo katika mashamba yao.
More Stories
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda