December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafugaji na Wananchi watakiwa kukutana kikao cha pamoja na menejimenti ya Kiwanda cha Sukari TPC

Na Martha Fatael, Moshi

MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ametaka uongozi wa kata ya Arusha chini, wilayani Moshi, wafugaji na wananchi kufanya kikao cha pamoja na menejimenti ya Kiwanda cha Sukari TPC Ltd kujadili hali ya kiusalama miongoni mwao.

Kauli hiyo inafuatia kuchomwa moto kwa nyakati tofauti kwa zaidi ya Hekta 44 za eneo la Namalog lililotengwa kwa ajili ya ufugaji wa wanyamapori kama sehemu ya Utalii kitandani hapo.

Babu amesema hayo wakati kamati ya usalama ya mkoa ilipotembelea eneo lililoathiriwa na moto uliochomwa na baadhi ya wananchi.

“Inawezekana Kuna jambo halipo sawa, uongozi wa Tarafa,kata,Kijiji Cha Mikocheni na wananchi na wafugaji nendeni mkafanye mazungumzo na TPC kujua tatizo ni Nini, Hawa TPC ni msaada mkubwa Sana Kwa vijiji jirani katika Miradi mbalimbali” amesema.

Babu amesema kamati ya usalama ya mkoa haijafurahishwa na kitendo Cha kuchomwa moto kwa eneo Hilo jambo ambalo linadhorotesha jitihada za uwekezaji.

“TPC wametenga eneo hili kwa ajili ya Utalii lakini Wana mpango wa kujenga hoteli ya kitalii ambayo itakuwa msaada pia kwa wananchi wa vijiji jirani ” amesema.

Mkuu wa Mkoa amesema anazo taarifa kwamba TPC hutoa malisho ya mifugo kwa wananchi wa vijiji jirani nyakati za kiangazi lakini pia Miradi ya Elimu,Afya na Miundombinu.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa, Kaimu Ofisa Mtendaji Utawala wa TPC, David Shilatu amesema tukio hilo ni la pili kwani la kwanza lilitokea Mei mwaka Jana ambapo Hekta 21 ziliteketea.

Amesema tukio la pili lilitokea Desemba 20 mwaka Jana ambapo Hekta 23 ziliteketezwa na moto unaosababishwa na watu wasiojulikana.