Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
VIKUNDI vya wafuga nyuki Wilayani Sikonge Mkoani Tabora vimeshukuru serikali ya awamu ya 6 kupitia Wakala wake wa Huduma za Misitu (TFS) kwa kuwawekea mazingira mazuri ya ufugaji nyuki katika maeneo ya misitu ya hifadhi.
Wakiongea na mwandishi wa gazeti hili aliwayetembelea hivi karibuni ili kujionea jinsi wanavyotekeleza majukumu yao wamepongeza ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa Maafisa Uhifadhi wa TFS na serikali kuwawekea mazingira mazuri.
Makamu Mwenyekiti wa Kikundi cha wafuga nyuki cha Miyombo kilichoko katika kata ya Misheni wilayani humo John Mkasiwa amesema wafuga nyuki wote kwa sasa hawana kikwazo chochote cha kufanya shughuli zao.
Amebainisha kuwa miaka ya nyuma walikuwa wanahangaika sana kupata vibali lakini sasa wamewekewa utaratibu mzuri, mtu au kikundi chochote wanapoomba hupata kibali kwa wakati na kuanza shughuli zao mara moja.
Aidha ameongeza kuwa hata wanapoingia katika misitu au mapori ya hifadhi wanapewa ushirikiano mzuri na wamekuwa sehemu ya walinzi wa misitu hiyo kwa kutoa taarifa kwa TFS punde wanapoona vitendo vya uharibifu na waharifu.
Mfuga nyuki Sara Moses ambaye ni Katibu wa Kikundi hicho amesema hadi sasa kikundi chao kina wanachama 56 na kina jumla ya mizinga 2,846 ya miti na maboksi na tangu waanze kazi hiyo wamepata mafanikio makubwa sana kiuchumi.
‘Tunaipongeza sana serikali inayoongozwa na mama yetu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa kwa vikundi vya wafuga nyuki kufanya shughuli zao katika misitu ya hifadhi pasipo bughudha yoyote’, amesema.
Boniface Kisamba mfuga nyuki, mkazi wa Madukani wilayani humo amesema wana kila sababu ya kumpongeza Rais Samia kwa kujali ustawi wa wananchi wake na kuruhusu vikundi vya wajasiriamali kufanya shughuli zao kwa uhuru.
Ameomba serikali kuwasaidia kupata masoko ya pamoja yatakayowawezesha kuuza mazao yao ya nyuki kwa bei nzuri, pia aliomba TFS kuwapunguzia gharama ya kuingiza vyombo vya usafiri kwenye hifadhi kwa ajili ya kubebea mazao hayo.
Afisa Uhifadhi wa TFS-Kitengo cha Nyuki, Wilayani humo Haji Abadllah ameeleza kuwa zaidi vya wafuga nyuki 40,000 wameshapewa vibali vya kufanya shughuli hizo na wote walipewa elimu ya ufugaji wa kisasa na utunzaji misitu.
Amebainisha kuwa wafuga nyuki ni marafiki wa TFS ndio maana wanawapa ushirikiano, hadi sasa kuna kambi zaidi ya 2000 za wafuga nyuki katika hifadhi hizo na wote wanaendelea na shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu.
Abdallah amefafanua kuwa ili kuhakikisha misitu hiyo inakuwa salama wanafanya doria za mara kwa mara na vikundi vyote vinavyofanya shughuli zao katika misitu hiyo vinawasaidia kulinda pia.
‘Wafuga nyuki wote wamepewa elimu ya ufugaji wa kisasa na wamesisitizwa kutumia vifaa sahihi vya uvunaji mazao ya nyuki na kutumia vizuri misimu ya mwaka ili shughuli zao zilete tija kubwa’, amesema.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 2 wafuga nyuki kutoka vikundi 4 vya Miyombo, Kitunda, Usunga na Kiyombo walipewa ruzuku ya kati ya sh mil 5 hadi mil 50 ili kuwainua zaidi katika shughuli zao.
More Stories
Serikali yahimiza wananchi kutembelea vivutio vya utalii
Magunia ya kufungia tumbaku yakamatwa
Madereva 16,Mwanza wafungiwa leseni ya udereva