December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara watakiwa kuzingatia ushirikiano na mataifa mengine

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

WAFANYABIASHARA nchini wameshauriwa kutumia kikamilifu fursa ya kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na mahusiano mazuri ya kiuchumi na mataifa mengine.

Aidha, amewashauri wafanyabiashara hao kuhakikisha wanatumia fursa ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nane za majaribio za kuuza bidhaa ndani ya Eneo Huru la Biashara Afrika ambalo litaanza Julai 1, mwaka huu, kwa kupeleka bidhaa zinazotakiwa bila kukaa wakisubiri wakisema watafanya.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam leo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt. Ashantu Kijaji kwenye Mkutano wa Wanyabiashara kuhusu kujenga uelewa na kuhamasisha kuchangamkia fursa za biashara chini ya mkataba wa eneo huru Afrika (AfCFTA).

Ametaka wafanyabiashara kuwekeza kwenye viwanda na kwenye biashara kwani Rais Samia amefanya kazi kubwa na ndiyo maana amechanguliwa kuwa kinara wa biashara Afrika kwa wanawake na vijana.

“Wanawake na vijana umefanya nini kumfanya Rais wetu kuwa kinara? Inabidi tukae tuzungumze kwa pamoja nini kinatukwamisha? Kwa nini tupeleke pamba nje badala ya nguo? Rais Samia ameamua, ni lazima tuamue kwenda kutoa huduma kimataifa,” alisema Dkt. Kijaji.,

Amesema Tanzania ni moja ya nchi nane za Afrika ambazo zimekubaliwa kuwa za mwanzo kunufaika Eneo Huru la Biashara Afrika kutokana na Rais Samia kufanyakazi kazi kubwa ya mahusiano ya kiuchumi.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara kujitafakari ili kuhakikisha wananufaika na bidhaa zinazotakiwa katika Eneo Huru la Biashara Afrika kwa kupeleka bidhaa zinazotakiwa na kutumia eneo hilo kikamilifu.

Amesema soko la Afrika ni muhimu sana kwa biashara na sasa masharti yamepunguzwa. “Tunaambiwa tupeleke bidhaa bila ushuru na kwa kiasi chochote maana yake nchi zote 54 za Afrika zinaongea lugha hiyo.

Kwa hiyo tusipoanza kupeleka sisi wao wataleta. Hatuwezi kujifungia kama kisiwa, lazima tushiriki kwa pamoja, tukisema tutapeleta, wao wataleta,” amesema Dkt. Kijaji na kuongeza,

“Wasafirishaji wanatakiwa kujua ni bidhaa gani zinatakiwa kutoka Misri kuja kwetu, twende kuzisafirisha bidhaa hizo kwa malori yetu wenyewe hadi hapa nchini, tusipofanya sisi wao wataleta.”

Amesema ni muhimu kuainisha vikwazo wanavyokabiliana navyo ili waweze kuvipatia ufumbuzi. “Ni lazima kujua ni nini tuzalishe ili kuweza kunufaika na soko kubwa la Afrika.

Uzuri wetu ni jiografia nzuri ya nchi. Kuna nchi nane tunazihudumia ambazo hazifikiwi na bahari. Tujiulize tunanufaikaje na hii fursa? Ni muhimu sana tufikiri kwa pamoja na tujiulize kwa pamoja tunanufaikaje na na fursa ya jiografia ya nchi yetu kama tunavyojiuliza tunanufaikaje na ardhi.”

Amesema Afrika ni bara lenye utajiri mkubwa, lakini bado wanaaminishwa kwamba bado ni masikini. Alisema asilimia 2.6 ya bidhaa ambazo nchi za Afrika zinapeleka duniani nyingi ni mali ghafi.

“Unapopeleka malighafi maana yake unawanyima watu wetu ajira. Unapopeleka malighafi nje ya nchi maana yake zinaenda kubadilishwa na kuwa bidhaa ambazo zikiletwa huku tunazinunua kwa kwa gharama kubwa,” alisema Dkt. Kijaji.

Amesema huu ni wakati wa kukaa kati ya Serikali na sekta binafsi na kutafakari kwa pamoja kwani wakiendelea kujifungia ndani tutabaki kulalamika.

Akifafanua zaidi, amesema mchango wa nchi za Afrika wetu kwenye biashara duniani ni asilimia 2 tu, hivyo wanatakiwa kukaa na kuzungumza kwa pamoja ili kujua nini wafanye.

Kwa upande wa Asia amesema wao wenye wamefika asilimia 52 na kwa nchi za Ulaya ufanyaji biashara wao kwa wao ni asilimia 72.

“Bado tuna safari ndefu ya kukuza pato la nchi zetu na Afrika kwa ujumla, ndiyo maana viongozi wakuu wa nchi zetu kwenye mkutano wao 18 uliofanyika Januari, 2022 nchini Ethiopia waliagiza kuanzishwa kwa mchakato wa Eneo Huru la Biashara Afrika,”alisema.

Ameishukuru sekta binafsi kwani tangu agizo hilo lilipotolewa ilianza kuangalia maeneo ya kunufaika na eneo huru la biashara Afrika.

Amesema kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara Afrika kutarahisisha wa wafanyabiashara kusafiri na mitaji ndani ya Bara ya Afrika bila vikwazo vyovyote.

“Pia kutaimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika. Mtanzania hazuiwi kutafuta mtu yeyote Afrika ili kuungana na kuweza kuzalisha bidhaa zenye viwango vinavyotakiwa ili kufikia soko la Marekani,” alisema Dkt. Kijaji.

Amewataka wafanyabiashara kujua viwango vya bidhaa zinazozalishwa tayari kwa kupeleka Afrika na duniani.

“Tunahitajika kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuzipeleka duniani.”

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na biashara, Ally Gugu amesema Tanzania ni sehemu rasmi ya Mkataba wa eneo huru la biashara la Afrika ambapo nchi wanachama pamoja na sekretarieti inayoendesha AfCFTA wamefanikiwa kuanzisha nyenzo inayotengeneza mazingira rahisi kwa walioibaini fursa kuwawezesha kuuza.

“Fursa hii ya Afrika kidogo ni nyepesi nguvu yetu ya kuipata tusiipoteze na tunaamini mnaweza kuitumia ipasavyo tukishirikiana na sisi”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Leodger Tenga amesema wapo tayari kuchangamkia fursa ya soko hilo linalokadiriwa kuwa na watu bilioni 1.4 lenye pato la pamoja ya thamani ya dola trilioni 1.2

“Lazma tupambane ili tufanikiwe hasa katika upande wa ubora wa bidhaa na tutaendelea kuhamasisha, kutoa elimu na kuwasaidia wanachama wetu waweze kufanya vizuri sokoni” Amesema Tenga.