Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Wafanyabiashara wa sekta ndogo ya mafuta wametakiwa kufanya biashara kwa kuzingatia sheria ikiwemo kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA).
Hayo yamezungumzwa na Mkaguzi Mwandamizi wa Mafuta EWURA Kanda ya Ziwa Mhandisi Nathaniel Uiso,wakati akiwasilisha mada katika semina ya wadau wa sekta ndogo ya mafuta ya petroli Mkoa wa Mwanza, ilioandaliwa na EWURA na kufanyika mkoani hapa.
Mhandisi Uiso,amesema ni makosa kisheria kufanya biashara ya mafuta bila ya kuwa na leseni ya EWURA,kwani faini yake ni milioni 20 hivyo ni vizuri kufanya biashara kwa kufuata sheria.
Amesema shughuli zote zinazohusu mafuta ya petroli ni lazima zifanyike kwa umakini na uangalifu mkubwa ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
“Ni muhimu kuzingatia na kufuata sheria,kanuni,viwango vya ubora na masharti ya leseni wakati wote,pia ni makosa kisheria kujenga miundombinu ya gesi ya kupikia bila kuomba na kupewa kibali cha ujenzi na EWURA,” amesema Mhandisi Uiso.
Kwa upande wake Meneja Ufundi Idara ya Petroli EWURA Mhandisi Shaban Seleman, amesema miundombinu mibovu ya kuhifadhia na kusafirishia mafuta ni hatari kwa usalama, mazingira, viwango na huweza kusababisha madhara makubwa kama vile kuharibika kwa ubora wa mafuta,kumwagika kwa mafuta ambayo hatimaye huweza kusababisha mlipuko wa moto na maafa makubwa kuweza kutokea.
Hivyo ili kujenga miundombinu ya mafuta ya petroli ni lazima kuomba kibali cha ujenzi kutoka EWURA.
Mhandisi Seleman amesema ni muhimu biashara ya mafuta ifanywe kwa kuzingatia kanuni na sheria,ambapo EWURA kwa kushirikiana na wadau imeandaa kanuni mbalimbali kwa ajili ya kusimamia sekta ndogo ya mafuta ya petroli hapa nchini.
Wafanyabiashara wanapaswa kuomba na kupata leseni ya EWURA kabla ya kuanza kufanya biashara katika sekta ndogo ya mafuta.
“Kwa mujibu wa sheria ya mafuta sura ya 392,wadau wanapaswa kuomba na kupata kibali cha ujenzi wa miundombinu ya mafuta ikiwemo vituo vya mafuta,wafanyabiashara wanapaswa kuomba leseni kabla ya kuanza kufanya biashara katika sekta ndogo ya mafuta,” amesema Mhandisi Seleman.
Naye Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa George Mhina, amesema semina hiyo lengo lake ni kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara hao wa sekta ndogo ya mafuta pamoja na kuona changamoto zilizopo ili kuweza kufanya sekta hiyo ina kua na kufika kila maeneo hususani vijijini.
“Sekta ya mafuta ni muhimu katika kukuza uchumi,tumekaa kwa pamoja na wadau ili kujua kwa namna gani tutaimarisha ushirikiano katika sekta pamoja na kujua changamoto zilizopo kujadili kwa pamoja ili mwisho wa siku gesi ya kupikia na mafuta viweze kupatikana kwa bei na mazingira rafiki,”amesema Mhina.
Awali akifungua semina hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, amewataka wafanyabiasha hao kuhakikisha wanazitambua,kuzielewa na mwisho wa siku kuzingatia sheria za sekta ya mafuta ili kuepuka kuzivunja hali ambayo inaweza kusababisha kutozwa faini au kufungiwa biashara zao.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia