November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara Kariakoo wawashika mkono waathirika Hanang

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji, amepokea msaada wenye thamani zaidi ya Shilingi milioni 60, kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) kwa ajili ya kusaidia waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope na mawe Hanang mkoani Manyara.

Mafuriko hayo yalitokea usiku wa kuamkia Disemba 3, mwaka huu na kusababisha maafa makubwa ikiwemo watu kadhaa kupoteza masisha.

Msaada huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Meya wa Jiji, Omary Kumbilamoto na Jumuiya hiyo, inayoundwa na Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kwa kushirikiana na Kijiwe cha Raha Square kilichopo ndani ya soko hilo.

Lengo la kutoa msaada huo ni kuunga mkono juhudi wa Serikalikufuatia janga hilo la kitaifa.

Miongoni mwa misaada iliyotolewa ni pamoja na mabalo 44 ya mavazi na kiasi cha pesa taslimu, ambazo bado zinaendelea kuingizwa kwenye akaunti ya mahafa.

Akipokea msaada huo, Waziri Kijaji amesema, msaada huo utawafikia moja kwa moja walengwa Disemba 15, mwaka huu, huku akitoa wito kwa wafanyabiashara wengine wa Kariakoo wanaoguswa kufikisha msaada wao eneo la Raha Square.

Pia, ametoa pongezi kwa wafanyabiashara hao na kuwataka kuendelea kuwa na moyo wa upendo na kizalendo, kwani maafa si jambo lililopangwa na binadamu.

“Nawapongeza sana wafanyabiashara wa Kariakoo kwa hili mlilofanya, hii inaonesha wazi kuwa unapoongelea biashara basi unaongelea Kariakoo iliyopo ndani ya Wilaya ya Ilala. Naomba muendelee kuwa na moyo huo wa upendo na kizalendo kwa watu wenye uhitaji.

“Wengi mliokuwa mnataka kujua mwisho wa zoezi la kuendelea kupokea misaada hii kwa ajili ya ndugu zetu wa Hanang, hivyo nasema tunaendelea kupokea hadi kesho saa 4 asubuhi na saa 5 tutakuwa tumeanza safari ya kwenda kuwaona ndugu zetu wa Hanang na siku ya ijumaa saa 6 tutaanza kutoa msaada huu kwa walengwa”, amesema Kijaji.

Aidha, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya, ikiwa pamoja na kuwa na ushirikiano mzuri na wafanyabiashara hao, jambo ambalo linaacha alama nzuri kwa Serikali.

“Nampongeza sana Kaka yangu Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye pia ni mlezi wenu wafanyabiashara kama mlivyosema, kwa hali hii inaonesha wazi kuwa kuna uhusiano mzuri kati yako na wafanyabiashara hawa, lakini pia naomba uendelee kusimamia vyema misaada hii inayoendelea kutolewa, itolewe hapahapa sehemu husika,” ameongeza Kijaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewapongeza wafanyabiashara wa Kariakoo kwa kuendelea kuonesha ushirikiano mzuri kwa Serikali, huku akitolea mfano ushiriki wao katika matukio mbalimbali ya kiserikali ikiwa pamoja na uhamasishaji wa ulipaji kodi.

Pia, amewataka wafanyabiashara hao, kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambazo ameendelea kuzifanya.

“Kwanza kabisa napenda kutoa salamu za pole kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maafa haya yaliyotokea huko Hanang kwa ushiriki wake, hivyo nawaomba ndugu zangu wafanyabiashara wa Kariakoo tuendelee kuunga mkono jitihada anazoendelea kuzifanyia Rais wetu.

“Niwapongeze sana kwa moyo huu mlioonesha wa kutoa msaada kwa wahanga hawa na kutambua kuwa suala la maafa ni suala la kila mmoja linaweza kumtokea,” amesema Mpogolo.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Justine Massawe, ametoa wito kwa wafanyabiashara hao, kuendelea kujitokeza kwa wingi kutoa msaada, ambapo amesema zoezi hilo litafika ukomo mapema kesho.