December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanya maandamano ya hiari kumpongeza Rais nyongeza ya mshahara

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Hivi karibuni serikali nchini hapa ilitangaza ongezeko la mshahara wa kima cha chini kwa wafanyakazi wa umma kwa asilimia 23.3, hivyo watumishi wa taasisi za serikali na mashirika ya umma mkoani Mwanza wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi hiyo ya kuwaongezea mishahara pamoja na kuwapandisha madaraja.

Pongezi hizo wamezitoa baada ya kufanya maandamano ya hiari kwa ajili ya kumpongeza Rais ambayo yameandaliwa na Shirikisho Huru la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA),Mkoa wa Mwanza na kupokewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel.

Akizungumza mara baada ya maandamano hayo kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Katibu wa TUCTA Mkoa wa Mwanza Zebedayo Athuman, ameeleza kuwa wafayakazi wa serikali,taasisi na mashirika ya umma wanampongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kuboresha maslahi yao na kuwaongeza mishahara kwa asilimia 23.3,kuajiri wengine wapya na kuwapandisha madaraja.

Zebedayo amesema,licha ya kuwafuta machozi watumishi na kuwapa furaha, bado watumishi wa sekta binafsi wana malalamiko ya kutoongezwa mishahara tangu mwaka 2013 na kikokotoo kwani nao wanastahili kuongezewa mishahara,wanaamini Rais atalipatia ufumbuzi jambo hilo.

“Mwanza tunatoa shukurani kwa Rais kwa nia ya dhati kwa jitihada zake za kuboresha maslahi ya watumishi,ametimiza ahadi yake aliyotoa Mei Mosi 2021, ndio msingi uliotusukuma kumpongeza,amepandisha madaraja watumishi 92,619, ameajiri wapya 12,336 wa sekta za elimu na afya,”amesema Zebedayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Gabriel amesema kitendo cha watumishi wa umma kumpongeza Rais Samia kimeonesha fadhila kwa mkuu huyo wa nchi.

“Jambo hili lina shangaza kwa sababu watu wengi wamezoea kulalamika na kudai badala ya kushukuru,niwaombe watumishi wa umma msiache kumweka kwenye maombi kutokana na kazi ngumu anayoyafanya ya kuleta maendeleo na kuboresha maslahi ya watumishi na wananchi,” amesema Mhandisi Gabriel.

Pia amewahimiza watumishi hao kufanyakazi ya kizalendo ya kuwatumikia watanzania kama wanavyofanya kwa Mungu, wakifanya hivyo watampa nguvu Rais Samia ya kuchapa kazi.

Sanjari na hayo aliwasihi wasijiingize katika vitendo vya wizi, ubadhirifu na vitendo vya rushwa kwani taifa lolote husimama kwenye haki na haki itembelee taasisi zote ziwahudumie wananchi kwa haki.

Baadhi ya watumishi wa taasisi za serikali na mashirika ya umma mkoani Mwanza, wakiwa katika maandamano ya hiari ya kumpongeze Rais Samia.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, akizungumza mara baada ya kupokea maandamano ya hiari ya kumpongeze Rais yalifanywa na watumishi wa taasisi za serikali na mashirika ya umma mkoani Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Katibu wa TUCTA Mkoa wa Mwanza Zebedayo Athuman, akizungumza mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel kupokea maandamano ya hiari ya kumpongeze Rais yalifanywa na watumishi wa taasisi za serikali na mashirika ya umma mkoani Mwanza na kuandaliwa na shirikisho hilo.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel wa pili kulia akiwa na Mwenyekiti TUCTA mkoa wa Mwanza Yusuph Simbauranga katikati wakati wakipokea maandamano ya hiari ya kumpongeze Rais yalifanywa na watumishi wa taasisi za serikali na mashirika ya umma mkoani Mwanza na kuandaliwa na TUCTA Mkoa wa Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)