Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma ametoa wito kwa jamii, wadau wa ndani na nje ya nchi, kuungana katika kuharakisha mabadiliko yanayohitajika ili kuwafanya wanawake na wasichana kuwa salama kutokana na madhara ya ukeketaji.
Wito huo ameutoa jana wakati wa kufunga mkutano wa kimataifa wa ukeketaji, uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es salaam ambapo amesema hakuna sababu ya kuendelea na ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kutokana na mila zenye madhara.
Aidha amesema mapendekezo yaliyotolewa katika mkutano huo yakitekelezwa vizuri yataokoa na kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya vitendo hivyo viovu katika mataifa mbali mbali.
Waziri huyo ametaja baadhi ya mapendekezo yaliyopendekezwa katika mkutano huo ikiwemo ushirikishwaji wa jinsia zote pamoja kuwajengea uwezo wavulana na wasichana kukataa ukeketaji, Tume ya Umoja wa Afrika kuratibu mikutano mikuu pamoja na Mawaziri wa Nchi Wanachama kukutana kwa karibu na ana kwa ana ili kubadilishana mbinu na njia bora za kukomesha ukeketaji.
“Hivyo kwa kuhitimisha mkutano wetu wa leo na kwa mikakati madhubuti ambayo tumejiwekea tunaenda kuona ” Mabadiliko katika Kizazi” yaani change in a Generation kuhusu kutokomeza Ukeketaji” Amesema Waziri Pembe.
Aidha Riziki ameishukuru Kamisheni ya Umoja wa Afrika na washirika wake kwa kuishirikisha nchi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu na kupitia juhudi za Mawaziri kutoka nchi zilizoshiriki ikiwemo Ethiopia, Ghana, Libya, Nigeria, Somalia, Uganda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Fatma Toufiq amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeandaa Mpango kazi wa Kitaifa wa kutokomeza ukeketaji pamoja na sheria ya mtoto ikiwa ni juhudi za kupinga vitendo hivyo.
Wakizungumza baadhi ya washiriki wa mkutano huo wameahidi kuyachukua na kuyafikisha mapendekezo yaliyotolea katika mamala ya nchi zao ili hatua ziweze kuchukuliwa katika kupambana na ukeketaji.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua