November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wakaribishwa kusaidia watoto wa kike mashuleni kupata vifaa vya hedhi salama

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali kuwasaidia watoto wa kike kupata vifaa vya hedhi salama ili viweze kuwasitiri na kuwafanya wajiamini wakati wa masomo bila kuathiri mahudhurio yao shuleni na kuwalinda na magonjwa.

Hayo ameyasema leo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah J. Kairuki wakati aliposhiriki mbio za hisani za “RUN FOR BINTI MARATHON 2023” zilizoratibiwa na Shirika la Legal Services Facility (LSF) kwa kushirikiana na Shirika la Smile for Community (S4C) zenye lengo la kukusanya rasilimali fedha kwa ajili ya Watoto wa kike kupata vifaa vya hedhi na kuwalinda na magonjwa.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaunga mkono jitihada zote za LSF na S4C kupitia mbio za ‘RUN FOR BINTI MARATHON’ nakuahidi kuweka mazingira bora ya upatikanaji na uzalishaji wa bidhaa za hedhi ili kuboresha sekta ya afya na pia sekta ya elimu nchini” amesema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya afya na elimu kuhakikisha inaboresha miundombinu ya afya na elimu kwenye mamlaka za serikali katika ngazi zote ikiwemo halmashauri, wilaya, mikoa mbalimbali nchini.

“Ni faraja kuona LSF na S4C wanaunganisha jitihada zao pamoja huku wakikaribisha wadau wengine katika mbio hizi ambazo manufaa yake yanakwenda kusaidia jamii hususani afya na usalama wa mtoto wa kike shuleni katika mikoa nufaika kwa mwaka huu”

Aidha, Waziri Kairuki amesema mbio hizo ni jitihada za kumuwezesha mwanamke kiuchumi kwani zitasaidia kupatikana kwa fedha zitakazosaidia kuwajengea uwezo wanawake na wasichana kupitia vikundi vyao vya kiuchumi ili waweze kutengeneza sodo (taulo za kike) ambazo zinaweza kutumika zaidi ya mara moja na kuziuza kwa bei nafuu katika jamii inayowazunguka.

Amesema Mikoa itakayonufaika na mbio hizo za hisani ni Lindi na Mtwara na inatarajiwa kuwanufaisha wanafunzi zaidi ya 15,000 pamoja na kikundi kimoja cha kiuchumi cha wanawake kutoka katika kila mkoa kitajengewa uwezo kupitia stadi za utengenezaji wa sodo ili kiweze kusaidia wengine.

Kadhalika, Waziri Kairuki amezipongeza taasisi na makampuni ya Total Energies, Dar Fresh, SGA, Tips, Water for People na wengine wanaoendelea kujitokeza kujenga ustawi na maendeleo ya mtoto wa kike na kumuwezesha mwanamke kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala amesema wamekuwa wakijikita katika upatikanaji wa Haki kwa wote hususani wanawake na watoto wa kike, suala la haki ya afya ya uzazi, kushiriki masuala ya uchumi, haki ya kushiriki kwenye masuala ya elimu, mtoto wa kike kutoingizwa kwenye ukatili wa kijinsia.

Hivyo kupitia Mbio hizo amesema zitasaidia kuhakikisha wanamkomboa mtoto wa kike kutoka kwenye mazingira hayo ili aweze kushiriki kikamilifu ili mtoto wa kike apate haki sawa na wenzao na kuweze kuja kuwa viongozi wa baadae.

“Tunategemea kuona mabadiliko katika jamii, haki ikitendeka na tunaamini mbio hizi pamoja na jitihada nyingine tunazozifanya kupitia watoa huduma za msaada wa kisheria tunaweza kuwafikia wengi sana na kushirikiana na wadau mbalimbali hususani serikali kupitia wizara mbalimbali tunaweza tukawafikia wengi zaidi nchi nzima.”

Ng’wanakilala amesema fedha ambazo zitakusanywa zitaenda kusaidia watoto wa kike ili waweze kuendelea na masomo yao na kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za jamii.

Nae, Mkurugenzi wa Smile for Community, Frola Njelekela amesema mbio hizo zimelenga kuboresha miundombinu ya shule hasa ujenzi wa vyoo rafiki kwa wasichana, kuboreshwa kwa miundombinu ya vyoo kusaidia uwepo wa mazingira bora kwa watoto wa kike na hedhi salama ili kukabiliana na milipuko ya magonjwa kwa wanafunzi mashuleni na kukuza afya bora.