November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau waitaka Sheria ya Afya ya Uzazi

Na Mwandishi wetu Timesmajira online

WAKATI duani ikiadhimisha siku ya Wanawake, Tanzania imetakiwa kutengeneza sheria itakayompa mwanamke nguvu ya kuamua kuhusu masuala ya afya ya uzazi.

Hali ilivyo sasa, inaelezwa kwamba nusu ya wanawake hapa nchini, hawafanyi uamuzi wao wenyewe kuhusu afya ya uzazi na uzazi.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam Machi 8,2024 na wadau wa afya ya uzazi wakati wa kilele cha siku ya Wanawake duniani ambapo Shirika la Marie Stopes Tanzania (MST), lilipokutanisha wadau kujadili changamoto za afya ya uzazi na mustakabili wa mwanamke.

Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile, amesema lazima ziwepo sheria zitakazompa mwanamke uwezo na nguvu ya kuamua kuhusu afya yake ya uzazi na uzazi.

Amesema pamoja na sheria hiyo hakuna budi mila na desturi chanya za kiafrika zinazomuandaa binti kuwa mwanamke zihimizwe kama ilivyokuwa awali.

“Miaka ya nyuma mila na desturi zetu waafrika zilimpa shangazi majukumu ya kumuandaa binti kwa kumfundisha miiko na jinsi ya kushiriki tendo bila kupata ujauzito hali iliyopunguza idadi ya mimba zisizotarajiwa na magonjwa.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa Young and Alive Initiative, Sesilia Shirima amesema inapaswa kuwepo na mkakati wa kuhakikisha wanawake wenye ulemavu na wagonjwa wa afya ya akili wanapata huduma zinazostahili za afya ya uzazi.

“Inasikitisha siku zote jamii inaamini kwamba mwanamke mwenye ulemavu wa miwili ama afya ya akili hawezi kushiriki tendo la ngono au ndoa… hii dhana ni kikwazo kwenye mapambano dhidi ya vifo vitokanavyo na uzazi.

“Wapo ndugu wakigundua binti au mwanamke wa hivyo amepata mimba wanamtoa kwa njia zisizo salama na kumsababishia matatizo na wakati mwingine kifo,” alisema Shirima.

Kwa sababu hiyo amewashauri watoanhuduma wa afya ya jamii kuwafikia wanawake wenye ulemavu wa mwili au akili pamoja na familia zao ili kuwapa elimu sahihi kwa kuwa mwanamke huyo mlemavu anazo hisia za kimwili.

Mkurugenzi wa Programu kutoka MST, Dk. Geofrey Sigala amesema licha ya kwamba ni haki kwa wanawake wote kupata huduma za afya ya uzazi na uzazi, wengi wao hulazimika kuomba ruhusa kwa mwenza wake.

“Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, nusu ya wanawake nchini Tanzania hawafanyi uamuzi kuhusu afya ya uzazi peke yao, lazima wawashirikishe wenzao wao.

“Kwa kuliona hili tunapaswa kuhakikisha wanawake huko walipo wanapata taarifa sahihi za afya ya uzazi kutoka kwa watoa huduma sahihi kwenye vituo vya kutolea huduma ama wale wa ngazi ya jamii ambao huwafuata wanajamii walipo,” amesema Dk. Sigala.

Mkurugenzi huyo aliwataka wanahabari kutumia vema kalamu zao kupeleka ujumbe sahihi wa afya ya uzazi unaotolewa na wataalam ili kuiponya jamii na vifo vitokanavyo na uzazi na saratani za shingo ya kizazi inayoteketeza wanawake wengi kila mwaka.

Wadau mbalimbali wakifuatilia mada za washiriki wa mkutano huo
Tike Mwambipile kutoka Chama Cha wanasheria wanawake Tanzania alishiriki pia mkutano huo.
Geofrey Sigala Mkurugenzi wa Programu kutoka Shirika la Marie Stopes Tanzania naye ni miongoni mwa walioshiriki mkutano wa kilele Cha siku ya wanawake Duniani