November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa Sanaa Seattle Kuupeleka Muziki wa Tanzania Kimataifa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online Seattle, Washington State, Marekani.

Muziki na sanaa nyingine za Tanzania vitapata fursa nyingine muhimu kuzidi kupaa kimataifa kufuatia mazungumzo yaliyofanyika kati ya wawakilishi wa Serikali ya Tanzania na wadau wa sanaa katika mji wa Seattle nchini Marekani.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini humo yakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi aliyeambatana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa nchini (Basata), Dkt. Kedmond Mapana, yatasaidia kuelekea kuutangaza muziki wa Tanzania nchini Marekani na duniani kwa ujumla.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Seattle Pacific (SPU) muelekeo mmojawapo ni kuutangaza muziki na sanaa nyingine za Tanzania kupitia Tamasha kubwa la Folklife linalofanyika Mei kila mwaka katika mji huo wa Seattle na jimbo la Washington kwa ujumla ambapo pia ndipo yalipo makao makuu au sehemu za makao makuu ya makampuni makubwa nchini Marekani kama Boeing, Amazon, Google, Bill and Mellinda Gates Foundation, Microsoft, Starbacks, kampuni ya Getty Images, Deloitte, Shirika la Ndege la Alaska na kampuni ya simu ya T-Mobile.

“Sehemu nyingine ya majadiliano ambayo wenzetu wamelipokea na kulikubali ni kushirikiana nao kuleta Tamasha la Serengeti (Serengeti Festival) kufanyika katika miji kadhaa ya hapa Marekani kama sehemu ya kuitangaza nchi yetu na kuunganisha sanaa na utamaduni wa nchi hizi mbili za Marekani na Tanzania na Afrika kwa ujumla,” alisema Dkt. Abbasi.

Baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo ni: Prof. Barbara Lundquist, Mtaalamu Mstaafu wa Muziki Chuo Kikuu cha Seattle Pacific na mwasisi wa taasisi ya Chamwino Connect inayosaidia shughuli za Sanaa Tanzania na kwingineko Afrika; Ben Hunter Mkurugenzi wa Masuala ya Wasanii katika Tamasha la Folklife; Simon Okello Mjumbe wa Bodi ya Folklofe Festival na Kiongozi wa Taasisi ya OneVibeAfrica.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni: Gabriel Solis, Mkuu mpya wa Idara ya Muziki na Historia ya Muziki, Chuo Kikuu cha Washington, Tim Sneath kutoka kampuni mashuhuri ya Google na Mwenyekiti wa sasa Chamwino Connect, Prof. Patrician Campbell kutoka Chuo Kikuu cha Seattle Pacific.