November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa Kidigitali waiomba,Serikali kuangalia sekta ya usafirishaji fedha mitandaoni kwa mapana

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

WADAU wa masuala ya kidigitali nchini wamemuoamba Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Selemani Jafo kuanza kuangalia kwa mapana zaidi sekta hiyo hasa upande wa usafirishaji fedha kidigitali yenye lengo la kuleta mabadiliko na kujenga jamii jumishi kwa maendeleo endelevu.

Akizungumza katika mkutano uliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ambao umemkutanisha Waziri Jafo na viongozi wa vyama vya biashara Tanzania, Makamu Rais na Meneja Mikakati Kampuni ya Airpay Tanzania, Mihayo Wilmore amesema ni muhimu serikali kuanza kuangalia upande mwingine wa ufanyaji biashara hasa katika sekta hiyo ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya mtandaoni.

Amesema anayasema hayo kwa sababu upande wa biashara za kidigitali hasa usafirishaji fedha kwa mtandao kuna changamoto ya kutotambuliki kama wafanyabiashara bali mafundi.

Wilmore amesema changamoto nyingine ni kutakiwa kufungua kampuni yenye ofisi kwenye Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ilihali hawahitaji kuwa na ofisi ili wafanye biashara.

Amesema kutokana na vikwazo mbalimbali soko hilo la biadshara mitandaoni limekuwa chini ukilinganisha na nchi zingine za Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

“Biashara za mitandaoni kwa takwimu zilizopo mwaka jana Kenya waliingiza Dola za Marekani Milioni 244 huku Tanzania ikiingiza Dola za Marekani Milioni tisa tu.

“”Tanzania tumepakana na nchi saba na nchi zote zinahudumiwa na bandari yetu ya Dar es Saalam lakini biashara ya fedha mtandaoni tupo chini kuliko wenzetu ambao wamepakana na nchi moja tu,” amesema Wilmore.

Aidha amesema Kampuni ya Airpay ambayo inahusika katika masuala ya Tehama hasa upande wa usafirishaji wa fedha kwa njia ya mtandao kwa sasa ipo katika nchi nne ambazo ni Tanzania, Zambia, DRC Kongo na Ghana.

Awali akifungua mkutano huo, Waziri Jafo ameagiza kupata taarifa ya kila sekta na maeneo wanayotaka yafanyiwe kazi ili kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini.

Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kumuandalia ratiba ya kila sekta ili akutane nao akiwa na Waziri wa sekta husika lengo likiwa ni kutatua kero zinazowakumba wafanyabiashara.

Amesema Tanzania ina fursa kubwa ya biashara katika nyanja mbalimbali na kama kuna vikwazo ijulikane nini cha kufanya ili mapato ya nchi yaongezeke.