Na Stella Aron, TimesMajira Online
WADAU wa habari nchini wameishauri Serikali kufanya mabadiliko kwenye utaratibu wa utoaji leseni kwa magazeti kwa kipindi cha kila mwaka badala yake warejee mtindo wa zamani wa usajili wa gazeti wa kudumu.
Hayo yamebainika kwenye mkutano ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa njia ya Mtandao wa Zoom ambapo mada kuu ilikuwa ikiangazia Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini yaliyowasilishwa serikali.
Wameshauri Serikali inapaswa kuiangalia kwa namna ya kipekee Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ili baadhi ya vipengele ambavyo vinaonekana kuwa kikwazo vifanyiwe maboresho, kwa kuwa kufanya hivyo watasaidia Sekta ya Habari kustawi kwa kasi.
Kwa hatua hiyo itawezesha kuchangia kukuza pato la Taifa, kufungua fursa za ajira kwa makundi mbalimbali zikiwemo rasmi na zisizo rasmi nchini.
Wamesema kuwa dhamira ya Serikali ya kutunga sheria na kanuni za kusimamia sekta ya habari ina nia njema kwa lengo la kuongeza ufanisi na ustawi bora, lakini kupitia sheria nne zinazosimamia habari zinahitaji maboresho katika baadhi ya vifungu ili kuepuka migongano ya maslahi, upendeleo, urasimu na wakati mwingine manyanyaso kwa wadau wa habari nchini.
Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 ambayo inasimamia radio, TV na Mitandao ya Kijamii, Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya makosa ya Mtandao ya 2015 zikiwemo kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018 ziliyogawanywa katika vipengele mbalimbali.
Wakili na mwanahabari, James Marenga akiwasilisha mada katika mkutano huo amesema, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ikiwemo Sheria ya Kupata Taarifa ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 kuna baadhi ya vifungu au vipengele ambavyo vina changamoto ambavyo vikifanyiwa mabadiliko vitawezesha sheria hizo kuleta ufanisi.
“Kuna umuhimu wa kuwa na sheria rafiki kwa vyombo vya habari kwa maendeleo ya nchi kwani kutungwa kwa sheria rafiki kwa vyombo vya habari kutawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria”amesema.
Amesema, miongoni mwa vifungu ambavyo vina mapungufu katika sheria hiyo ni pamoja na 4 (1), 5 (1), 6(1),7(1), 7(3), 9, 11, 22(1) na 22(2) ambavyo vinazungukwa na neno “Intentionally” (kwa kudhamiria).
“Kuna umuhimu wa kurekebisha sheria na kufuta neno “kwa kudhamiria”. Haiwezekani kuthibitisha nia ya kufanya uhalifu kwa maneno ya kubahatisha,”amesema.
Naye mwenyekiti TEF Deodatus Balile ameshauri kuwepo kwa sheria ya adhabu ya miezi sita jela kwa kampuni zitakazoshindwa kulipa fedha za matangazo kwa vyombo vya habari ndani ya siku 30 huku akipinga kifungu kinachompa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), madaraka ya kuratibu matangazo yote.
Balile amesema ili vyombo vya habari vifanye kazi kwa uhuru lazima baadhi ya vifungu viondolewe na utaratibu wa utoaji leseni kwa magazeti umechangia kufifisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
“Mfano tumeshuhudia kusitisha leseni za magazeti ya Mwanahalisi, Mseto, Mawio na kufuta Tanzania Daima, je utaratibu huu una faida yoyote zaidi ya kuua uhuru wa vyombo vya habari.
“Je, kwa nini tusirudi katika utaratibu wa zamani ambapo gazeti lilikuwa linasajiliwa na kujiendesha bila kufutwa kama ilivyo sasa? mazingira yakiwa vizuri, sheria zikawa nzuri, matangazo yakatolewa kwa bei stahiki badala ya sasa ambapo wanashusha bei watakavyo, mapato ya vyombo vya habari yataongezeka,” amesema.
More Stories
Rukwa waanzisha utalii wa nyuki
Mhandisi Kundo ataka vyanzo vya maji vitunzwe
Dkt.Kazungu:Megawati 30 za Jotoardhi kuingia kwenye gridi ifikapo 2026/27