January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau Serikali za Mitaa wapewa somo

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online Dodoma

TAASISI ya Uongozi nchini  imewakutanisha wadau wa Serikali za Mitaa katika Mkutano uliolenga kuhamasisha Utawala bora ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa umma.

 Akifungua mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi na kufanyika jijini Dodoma ,Naibu Waziri ,Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Festo Dugange amewataka wadau hao wa Serikali za Mitaa kuwa wabunifu lakini pia kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi na kuleta matokeo chanya katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili.

Amewataka wadau hao kuhakikisha viongozi waliochaguliwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka huu ,wanafanya kazi kwa bidii na kutatua kero na kitoanhuduma bora kwa wananchi .

“Ni matarajio ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ,lakini pia no matarajio ya Rais mwenyewe kwamba,waliochaguliwa wanakwenda kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa .”amesema Dkt.Dugange

Aidha amesema katika kuleta ufanisi kumekuwa na changamoto za mifumo ya kiera kisheria na kitaasisi huku akiwataka wadau hao kutoa maoni ili kuboresha katika maeneo hayo kwa lengo la kuleta ufanisi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa .

Amewataka wadau hao kusimamia mapato ya ndani ya Halmashauri lakini pia kuibua vyanzo jipya na kukusanya fedha kwa ufanisi zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri nchini badala ya kutegemea fedha kutoka serikali Kuu.

“Ugonjwa uliopo katika Halmashauri nyingi nchini ni asilimia kubwa ya fedha za miradi ya maendeleo zinatoka Serikali Kuu ,uhalali wa uwepo wa halmashauri uko wapi,

“Ni muhimu tukae ,tufanye tathmini ,tujifunze tuone maeneo tunayoweza kuyaboresha ili tutoke kwenye utegemezi wa Serikali Kuu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani.” Amesema Dkt.Dugange 

Aidha amesema ,kwa upande wa Serikali Kuu imekuwa ikitoa fedha ambapo katika kipindi cha mwaka 2023/2024, Ofisi ya Rais TAMISEMI ,taasisi zilizo chini yake, mikoa 26 ikijumuisha halmashauri 184 ziliidhinishiwa bajeti ya trilioni 9.18, kati ya fedha hizo, trilioni 3.53 zilienda kwenye miradi ya maendeleo na trilioni 5.65 zilikuwa ni za matumizi ya kawaida.

 Pia amesema serikali imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kusimamia misingi ya Viongozi wa Serikali za Mitaa (Madiwani, Wakurugenzi, na watumishi wote), ambapo watazingatia kanuni za maadili na uadilifu ili kuongeza kasi ya utendaji kazi wa Serikali hizo za Mitaa.

Aidha amesema hadi kufika Machi, 2024 Ofisi ya Rais-TAMISEMI na taasisi zilizo chini yake ilikusanya na kupokea trilioni 6.99 sawa na asilimia 76.18 ya fedha zilizoidhinishwa.

Naibu Waziri huyo alifafanua kuwa Kati ya fedha hizo, trilioni 4.47 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na trilioni 2.52 kwa ajili ya miradi ya maendeleo hasa katika sekta ya afya na elimu na kuendeleza ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya mikoa ikiwemo majengo ya utawala, makazi ya viongozi na watumishi wa mikoa, wilaya na tarafa.

Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo,  amesema katika mkutano huo kutakuwa na mawasiliano ya mada mbalimbali yakiwamo kuhamasisha Utawala Bora ili Kuongeza Ufanisi katika Utoaji Huduma kwa Umma.

Amesema wasilisho jingine ni uchambuzi wa hali halisi ya serikali za mitaa nchini ambapo yatajadiliwa kwa kina na Wadau hao.