WADAU mbalimbali katika sekta ya viwanda nchini wamekutana ili kujadili juu ya uundaji wa sera rafiki na kanuni zitakazosaidia kuimarisha biashara ya uzalishaji viwandani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wa wadau hao ulioandaliwa na Taasisi ya Liberty Sparks, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa taasisi hiyo, Evans Exaud alisema lengo lao ni kuwezesha uagizaji na usafirishaji wa bidhaa za viwandani bila matatizo, hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi wa Tanzania na ushindani wake katika soko la dunia.
Amesema mkutano huo ni sehemu muhimu ya mradi wa Ujirani Mwema, ambao sasa upo katika awamu yake ya pili na kwamba katika awamu hiyo wanalenga kupitia na kutoa mapendekezo ya kuboresha biashara ya kilimo, biashara ya uzalishaji viwandani, na sekta ya madini katika nchi ya Tanzania.
“Safari yetu ilianza na awamu ya kwanza ya mradi huu, ambapo tuliwashirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo mashirika ya serikali na wizara kama vile Wabunge, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uchukuzi na kikundi kazi. Mashauriano haya ya awali yalikuwa muhimu katika kuweka msingi wa kazi tunayoendelea nayo leo.
“Tunapoingia katika awamu ya pili, wigo wa ushirikiano wetu unapanuka zaidi. Sasa tutashirikisha wizara za ziada, kama Wizara ya Nishati na Madini pamoja na ofisi ya Waziri Mkuu, kuhakikisha kuwa mapendekezo yetu yanakuwa ya kina na yatakayosaidia kushughulikia changamoto na fursa mbalimbali ndani ya biashara ya uzalishaji viwandani na zaidi,” amesema Exaud
Aidha amesisitiza kuwa nguvu ya taifa hili ipo katika uwezo wa watu kufanya kazi kwa pamoja katika sekta mbalimbali, viwanda na mipakani hivyo ni muhimu wadau hao kukutana na kujadiliana changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi na wahusika.
Kwa upande wake Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Kitengo cha Biashara, Samwel Wangwe alisema bado kuna changamoto zinazokabili sekta hiyo ya biashara viwandani ikiwemo upande wa ubovu wa miundombinu, vifungashio hafifu, bidhaa kutokuwa na ubora, upatikanaji wa fedha na masoko kwa ajili ya kuuzia bidhaa.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato