Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) latoa muda wa mwezi mmoja kwa wadaiwa sugu kulipa madeni na watakaokaidi maagizo hayo watatangazwa katika vyombo vya habari ili Mashirika, makampuni mengine yasiingie kwenye makubaliano ya kibiashara na mtu au kampuni inayodaiwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 15, 2023 Jijini Dar es Salaam Meneja wa Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya amesema Shirika limeingia mikataba na Wapangaji ya kuwaruhusu kulipa madeni yao kwa awamu kila mpangaji anayodaiwa na kama ana sababu maalum ahakikishe anaweka utaratibu madhubuti wa kulipa madeni yake anayoidaiwa.
Aidha, Kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba (active tenants) ambao watashindwa kulipa kodi na malimbikizo yao ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa Saguya amesema atakuwa ameonyesha kuwa haihitaji nyumba anayopanga na Shirika litavunja mikataba yao ya upangaji na kuwaondoa kwenye nyumba kwa mujibu wa sheria.
Amesema Shirika linawasihi wapangaji watekeleze wajibu wao ili kuepuka usumbufu utakaoweza kujitokeza kwa kushindwa kutimiza wajibu huo na kuanzia sasa Mpangaji yeyote mpya hawezi kupangishwa bila kulipa amana ya pango (security deposit) ya miezi mitatu. Hii itasaidia Shirika kuzitumia amana(deposits) hizo pale wanapoacha madeni na kuondoka kwenye nyumba.
Amesema kwa wapangaji ambao walishapewa notisi mbalimbali za kulipa kodi wanayodaiwa, utekelezaji wa notisi hizo unaendelea kama notisi hizo zinavyoelekeza.
Muungano amesema Shirika linawashukuru wapangaji wote wanaotimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya nyumba kwa wakati kama mikataba ya upangaji inavyoelekeza na Shirika linawashukuru wapangaji walioitikia wito wa kwa kulipa madeni yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimamizi wa Miliki, Elias Msese amesema kuwa wadaiwa sugu watakaokaidi watakuwa wameruhusu Shirika kuwatangaza katika vyombo vya habari ili Mashirika na makampuni mengine yasiingie kwenye makubaliano ya kibiashara na mtu au kampuni inayodaiwa.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa