Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Shirika la Nyumba Taifa (NHC), limesema lipo kwenye mikakati mizito ya kutatua kero za wadaiwa sugu waliopanga kwenye nyumba zinazomilikiwa na shirika hilo.
Mikakati hiyo, ikiwemo kuwapeleka kwenye Kampuni inayoshughulika na ukusanyaji wa madeni ya wadaiwa sugu inayoitwa Credit Information Beuro (CIB).
Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya Habari hapa nchini leo, katika semina maalum ya kujengeana uwezo juu ya majukumu wanayofanya NHC, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Hamad Abdallah alisema, lengo la kufanya hivyo ni kulifanya Shirika kukusanya kiwango kikubwa ili kuipa serikali faida.
“Ukiangalia ukusanyaji wa kodi mpaka Juni mwaka, tumekusanya wastani wa asilimi 101, maana yake tunakusanya ‘Autstanding Rent’ ya madeni yetu. Na shirika moja ya maeneo ambayo yamekuwa na shida ni ulipaji wa madeni.
“Sasa hivi tuna madeni takribani bilioni 23.8 ambayo tunayodai na mchanganuo wa haya madeni ni, sisi tuna nyumba ambazo ni za makazi na biashara, sehemu ya madeni yetu yapo kwenye maeneo ya biashara,” amesema Abdallah.
Abdallah amesema, takribani bilioni 20.2 zipo kwenye biashara, makazi bilioni 3.3, lakini vile Shirika hilo limeweka kuweka mchanganuo kidogo.
Amesema, katika wapangaji walionao wapo wa binafsi na makampuni, taasisi za umma lakini pia wana Wabia.
“Asilimia 38 ya madeni yetu tunawadai wapangaji binafsi, lakini makampuni haya ni maeneo ya biashara zaidi ni asilimia 36, taasisi za umma asilimia 14,” amesema.
Hata hivyo amesema, zamani walikuwa na tatizo kwa sababu taasisi za umma zilikuwa zinadaiwa zaidi lakini kwa sasa wana nidhamu ya hali ya juu katika ulipaji.
“Wabia ni asilimia 12, awali tulikuwa tunadai ukiangalia mwaka wa fedha uliopita tulikuwa tunadai bilioni 28, kwa hiyo katika kipindi cha hivi karibuni ndani ya mwaka mmoja tumeweza kukusanya bilioni 5. kutoka kwenye hayo madeni na ndio maana tumebaki na deni la Bil.23,” amesema.
Mkurugenzi huyo alitaja mikakati ya kufanya kuhusu ukusanya wa madeni hayo kuwa, shirika limeingia mikataba na baadhi ya wadaiwa ambayo inawataka walipe ankara zao za sasa ili zisiweze kuwaathiri. Mbali na ule mkataba walionao lakini wameingia mkataba mwengine na hao wadaiwa.
Lakini kwa wale ambao hawawezi hata kulipa hiyo mikataba mingine ambayo shirika wameingia nao watavunja na kuchukua hatua nyingine za kisheria ili kulipwa madeni yao.
Mbali na hivyo, Pia Abdallah amesema NHC inafikiria wale wote ambao ni wadaiwa sugu watawatangaza kwenye vyombo vya habari ili watanzania wawatambue.
Aidha, Abdallah amesema Shirika hilo limeingia Mkataba na Kampuni inayoitwa Credit Infomation Beuro.
“Hawa ambao tutawatangaza wadaiwa sugu athari yake ni nini, watajikuta hawawezi kupata tena mikopo kwenye mabenki, ili waweze kupewa mkopo watafanyiwa uchunguzi kama tulivyofanya sisi kwa wabia kwenda kwenye kwampuni ya (CIB).
“Kwa hiyo, mbali ya kuipeleka kwenye vyombo vya habari lakini pia tutaipeleka kwenye Kampuni ya Credit Information Beuro. Kwa hiyo wadaiwa sugu kupitia semina hii warudi waanze kulipa madeni yao kwa sababu athari yake itakuwa kubwa,” amesema.
Amesema, kukwepa deni la NHC linaweka kumpatia mpangaji asari kubwa zaidi ni bora warudi waangalie jinsi gani wakakaa na kulipa.
Katika hatua nyingine, Abdallah amesema kwa mpangaji mpya, hawezi kupata upangaji bila ya kulipa Scurity Deposite (Amana ya Pango), kwa sababu zamani walikuwa nayo lakini ilikuwa na shida kwenye ufuatiliaji, hivyo kwa sasa wana mfumo mpya ambao umeweka udhibiti mwingi.
“Huwezi kuingia kwenye nyumba bila kulipa hizo amana za pango, kwa sababu hatuwezi kukupangisha bila ya kujua mwenendo wako, ndia maana unaanza kutanguliza pesa hiyo. Hatujui kama una uwezo wa kuitunza hiyo nyumba vizuri.
“Kwa hiyo inakuwa kama pesa ya tahadhari ambayo baada ya upangaji wako kuisha utarejeshewa hiyo pesa endapo umelipa kodi zako vizuri na hiyo nyumba uliitunza vizuri,” amesema.
More Stories
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo
TAKUKURU,yasaidia kurejesha hekali 8