January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachimbaji wadogo watakiwa kufichua watorosha madini

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

VIKUNDI vya wachimba madini Wilayani Igunga Mkoani Tabora vimetakiwa kuisaidia serikali katika kukabiliana na wimbi wa utoroshaji madini kwa kufichua wale wote wanaofanya vitendo hivyo.

Agizo hilo limetolewa juzi na Waziri wa Madini Dkt Dotto Biteko alipotembelea vikundi vya wachimbaji wa dhahabu katika kijiji cha Bulangamilwa wilayani humo ili kujionea namna wanavyofanya shughuli zao.

Amebainisha kuwa serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini ili wachimbaji wadogo na wakubwa waweze kufanya shughuli zao katika mazingira bora ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini.

Amesisitiza kuwa Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan anawapenda wachimbaji wadogo na anawathamini sana na anataka kuona changamoto zozote walizonazo zinamalizwa kwa haraka.

Waziri ameongeza kuwa Rais ametoa fursa kwa wananchi kuchimba madini hayo na kuuza ili kujipatia kipato na kuchangia pato la serikali tofauti na hali ilivyo sasa ambapo baadhi yao wamekuwa wakichimba na kuuza kimaficho.

Amewakumbusha kuzingatia kanuni za usalama wakati wote wanapotekeleza shughuli za uchimbaji ikiwemo kufuata taratibu na sheria za uchimbaji ili kuepusha katika maeneo ya migodi.

Aidha Waziri Biteko ameagiza wamiliki wa leseni na wasimamizi wa machimbo kujali maisha ya wachimbaji wadogo ili waweze kupata kipato kizuri ili kuwainua kiuchumi na kubainisha kuwa biashara hiyo ina matatizo ya kiutawala na uelewa.

Ameongeza kuwa migogoro baina ya wawekezaji na wananchi katika sekta ya madini imewafanya wawekezaji kupata hofu ya kuwekeza katika uchimbaji wa madini kwa baadhi ya maeneo hivyo kupunguza uzalishaji wa madini.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kujenga mahusiano mazuri na wawekezaji ili kutatua changamoto zinazojitokeza kati yao ili wawekezaji waweze kutekeleza huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yanayozunguka migodi.

Mmiliki wa mgodi huo Rashid Shaboot amesema tangu waanze uzalishaji mwezi Februari mwaka huu wameweza kuzalisha jumla ya kilo 48 za dhahabu zenye thamani ya sh bil 6.3 hivyo kuwezesha serikali kupata mrabaha wa sh mil 383.8.

Ameshukuru ushirikiano mzuri wanaopata kutoka serikali ya wilaya hiyo kwa utayari wao wa kutatua changamoto zinazoibuka baina ya wachimbaji na wamiliki wa leseni, aidha aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ili kufanikisha utekelezaji miradi ya maendeleo.